Joy FM
Joy FM
22 May 2026, 09:15

Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza imeendelea kuchukua hatua za kuongeza ushiriki wa makundi maalum katika zabuni na tenda za serikali kupitia mfumo wa manunuzi ya umma wa NeST, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotolewa na serikali.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza leo. Akitoa mada katika mafunzo hayo, Mwezeshaji kutoka PPRA Kanda ya Kati na Magharibi, Eng. Mohamed Ulenga, amesema serikali imetenga asilimia 30 ya zabuni kwa ajili ya makundi maalum ili kuyawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi kupitia mfumo wa manunuzi ya umma.

Amesema mfumo huo umefungua fursa nyingi kwa vikundi hivyo, ikiwemo uwezo wa kushiriki na kupata tenda hata kutoka maeneo yaliyo nje ya mikoa yao huku akisisitiza umuhimu wa kutumia vikundi vya mfano vitakavyosaidia kuongeza uelewa na hamasa kwa vikundi vingine kujiunga na mfumo huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Uvinza Godfred Nkuba, amesema halmashauri imejipanga kuhakikisha vikundi vingi zaidi vinafikiwa, kusajiliwa na kuingizwa moja kwa moja kwenye mfumo wa zabuni za serikali ili viweze kujitegemea kiuchumi na kushiriki katika ushindani wa fursa mbalimbali za kibiashara.

Naye Kaimu Afisa Manunuzi wa Halmashauri hiyo, CPSP Jackson Kija, amesema bado kuna haja ya kuongeza elimu kwa makundi maalum kuhusu fursa ya asilimia 30 ya zabuni wanazopewa na serikali, huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na mitaji ya kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa tenda watakazopata.
Aidha, ameshauri vikundi kuanza kwa kushiriki tenda ndogo zenye uhitaji mkubwa kama huduma za usafi katika masoko na vituo vya afya, akieleza kuwa maeneo hayo yana fursa nyingi na yanaweza kuwa mwanzo mzuri wa kujijengea uwezo wa ushindani.

Mpaka sasa, Wilaya ya Uvinza imesajili vikundi 25 vya makundi maalum, huku vikundi viwili tayari vikiwa vimeunganishwa kwenye mfumo wa manunuzi ya serikali chini ya PPRA.
Hata hivyo, Halmashauri inaendelea na jitihada za kufikia lengo la kitaifa la kusajili vikundi 150 kwa kila Wilaya nchini.