Joy FM

Vijana Kasulu wapata ujuzi ufugaji wa samaki na uchakataji

16 July 2026, 15:37

Picha ya pamoja ya Mtendaji mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi FETA Tanzania na baadhi ya vijana waliohitimu mafunzo hayo. Picha na Hagai Ruyagila

Vijana ni nguvu kazi muhimu katika maendeleo ya taifa na ili waweze kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi, wanahitaji elimu na ujuzi unaowawezesha kujiajiri na kuanzisha shughuli za uzalishaji

Na Hagai Ruyagila

Jumla ya vijana 43 kutoka wilaya tatu za Mkoa wa Kigoma, ambazo ni Kasulu, Kibondo na Buhigwe, wamehitimu mafunzo ya ufugaji wa samaki na uchakataji wa mazao ya samaki yaliyotolewa na Chuo cha FETA Kigoma. Washiriki hao wametakiwa kuyatumia maarifa waliyoyapata ili kujinufaisha kiuchumi na kuchangia maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Mtendaji mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi FETA Tanzania, Dkt. Semvua Mzighani na baadhi ya viongozi wa Chuo Cha FETA Tawi la Kigoma na viongozi wa Chuo Cha Mati Mubondo wakitazama mabwawa ya samaki yakiandaliwa kwa ajili ya ufugaji wa samaki katika chuo Cha Mati Mubondo. Picha na Hagai Ruyagila

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo ya siku tatu yaliyofanyika katika Chuo cha Mati Mubondo Halmashauri ya Mji Kasulu, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Tanzania, Dkt. Semvua Mzighani, amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuongeza ujuzi wa vijana na kuwajengea uwezo wa kujiajiri.

Amewasisitiza washiriki kuyatumia maarifa hayo kuwafundisha wengine ambao hawakupata fursa ya kushiriki, hatua ambayo itasaidia kuongeza uzalishaji wa samaki, kuimarisha usalama wa chakula na kuinua uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.

Sauti ya Dkt Semvua Mzighani

Mkuu wa Chuo cha FETA Tawi la Kigoma, August Shirima, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha vijana kujiari na kupata ujuzi wa kisasa wa ufugaji wa samaki na uchakataji wa mazao yake ili waweze kuanzisha shughuli za uzalishaji zenye tija na kujiongezea kipato.

Sauti ya August Shirima

Mratibu wa Mradi kutoka Enabel Wilaya ya Kasulu, Abel Mbilinyi, amesema ushirikiano kati ya Enabel na FETA unalenga kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi hivyo amesema watawafuatilia vijana hao ili kujua menendo wao baada ya mafunzo hayo.

Sauti ya Abel Mbilinyi

Akisoma taarifa ya mafunzo hayo, Mkufunzi Bi, Rudia Shimba, amezungumzia idadi ya washiriki na namna walivyopata mafunzo ya nadharia na vitendo yatakayowawezesha kuanzisha na kuendesha miradi ya ufugaji wa samaki kwa ufanisi.

Mkuu wa Chuo Cha FETA Tawi la Kigoma August Shirima. Picha na Hagai Ruyagila

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema yamewasaidia kuongeza maarifa mapya ya kuanzisha miradi ya ufugaji wa samaki na uchakataji mazao ya samaki.