Joy FM
Joy FM
24 April 2026, 09:20

Kudumisha usafi wa mazingira ni jukumu la kila mtu, na ni njia rahisi ya kuhakikisha afya njema na maisha bora kwa wote.
Na Mwandishi wetu
Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe wamefanya zoezi la usafi wa mazingira katika Hospitali ya Wilaya, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuadhimisha Siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Zoezi hilo limeongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Mhe. Kanali Michael Ngayalina, pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya Bi. Utefta Mahega, ambao wameshirikiana bega kwa bega na watumishi katika kusafisha maeneo mbalimbali ya hospitali. Ushiriki wao umeonesha dhamira ya uongozi katika kuhimiza uwajibikaji na uzalendo miongoni mwa watumishi wa umma.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkuu wa Wilaya ameeleza kuwa usafi wa mazingira ni jambo la msingi katika kulinda afya za wananchi, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea maadhimisho ya kitaifa yenye umuhimu mkubwa kwa Watanzania. Amesisitiza kuwahamasisha wananchi pia kushiriki katika zoezi Hilo.
” Nawasisitiza vijana mjitahidi kufatilia historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ili muweze kuelewa umuhimu wa Muungano huu. Pamoja na Hilo nawashauri kila mmoja wetu apande walau mti mmoja wa matunda katika mazingira yake ili kuienzi siku hiyo muhimu” amesema Mhe. Kanali Michael Ngayalina.

Kwa upande wake, Katibu Tawala, Utefuta Mahega amesema kuwa Serikali imeagiza maadhimisho ya siku ya Muungano yafanyike kwa vitendo kupitia shughuli za kijamii, ikiwemo kufanya usafi wa mazingira, kupanda miti pamoja na kushiriki michezo mbalimbali.

Zoezi hilo linaakisi juhudi za Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe katika kuunga mkono maadhimisho ya Siku ya Muungano kwa vitendo, kwa kulenga kuboresha mazingira na huduma kwa wananchi.