Joy FM
Joy FM
12 December 2025, 18:11

Wadau mbalimbali wa masuala ya ukatili wa kijinsia kwa kushirikiana na Serikali wametakiwa kuendelea kutoa elimu na mikakati ya kukabiliana na vitendo vya ukatili
Na Hagai Ruyagila
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa, amewataka wadau wa maendeleo kuendelea kutoa elimu ya malezi kwa jamii, hususan elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, ili kuhakikisha wazazi na walezi wanalea watoto wao katika misingi sahihi itakayochangia ukuaji bora wa mtoto.
Akizungumza katika kongamano la kilele cha Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia lililoshirikisha watumishi wa umma, taasisi binafsi na viongozi wa dini, katika ukumbi wa chuo cha ualimu Kasulu TTC Rugwa amesema ushirikiano wa karibu kati ya wadau mbalimbali utaongeza ufanisi katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na kuimarisha uelewa wa pamoja ndani ya jamii.

Amesema kuwa malezi sahihi pamoja na kuzingatia maadili mema kutoka kwa wazazi na walezi ni msingi muhimu wa ukuaji mzuri wa mtoto.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Kigoma, Msafiri Nzunuri, amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia vimeendelea kupungua kutokana na juhudi za serikali na wadau wa maendeleo kutoa elimu kwa jamii kupitia kampeni na programu mbalimbali za uhamasishaji.

Mkuu wa dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kigoma, Mrakibu msaidizi wa Jeshi la Polisi Michael Mjema amesema licha ya kupungua kwa baadhi ya matukio ya ukatili, lakini vitendo hivyo bado vipo, hivyo jeshi la polisi kitengo cha dawati la jinsia na wadau wa maendeleo wameendelea kutoa elimu ili kuvitokomeza kabisa
Baadhi ya wananchi walioshiriki katika kongamano hilo akiwemo Theresia Mohamed na Lazaro Simon wamesema wanaotoa taarifa na wapo ambao hawatoi taarifa hivyo elimu endelevu kwa jamii ni muhimu ili kupunguza au kutokomeza vitendo vya ukatili, jambo litakalosaidia watoto kupata malezi bora kutoka kwa wazazi na walezi.

Kongamano la kilele cha Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia limebebwa na kaulimbiu isemayo “Tuungane, Kutokomeza ukatili wa kijinsia mitandaoni”