Joy FM

Wavamizi wa misitu ya Mkuti watakiwa kupisha ifikapo julai 2026 Kasulu

20 June 2026, 22:10

Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro, Picha na Mtandao

Baadhi ya wakazi wanaoishi maeneo hayo wameonesha kutii agizo la Mkuu wa Mkoa Kigoma huku wakiiomba Serikali kuhakikisha inasogeza huduma zote muhimu katika eneo hilo.

Na Mwandishi wetu

Serikali Mkoani Kigoma imewataka wananchi waliovamia Hifadhi ya Misitu ya Mkuti na kuishi kwenye vitongoji visivyo rasmi vya Kacheli na Lugufu relini katika Kijiji cha Zeze Wilayani Kasulu mkoani hapa, kupisha maeneo hayo ifikapo mwishoni mwa Julai, 2026.

Wavamizi hao wanaoishi kwenye zaidi ya kaya 900 tayari wamekwisha tengewa eneo katika Kijiji cha Zeze katika Kitongoji cha Landani, ambapo mpaka kufikia Juni 20, 2026 jumla ya kaya 364 zimeridhia kuhamia katika eneo jipya na kukabidhiwa viwanja kwa ajili ya makazi.

Akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua Hifadhi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amesema Serikali imeshajenga Shule katika eneo lililotengwa huku akimuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kasulu kuboresha eneo hilo kwa kuweka miundombinu ya barabara pamoja na kusogeza karibu huduma ya Maji.

Aidha baadhi ya wakazi wanaoishi maeneo hayo wameonesha kutii agizo la kiongozi hiyo huku wakiiomba Serikali kuhakikisha inasogeza huduma zote muhimu katika eneo hilo.

Awali akitoa taarifa kuhusu hali ya umiliki na matumizi ya eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu amesema maeneo ya Kacheli na Lugufu relini yapo chini ya Wakala wa Usimamizi wa Misitu (TFS) tangu mwaka 1956 na wananchi hao walitakiwa kupisha tangu mwaka 2022.

Amesema Sambamba na ujenzi wa shule, Serikali pia imewatengea eneo la makazi, Kilimo na mifugo.