Joy FM

Wazazi wenye mahitaji maalum watakiwa kuchukua tahadhari ya Ebola

1 June 2026, 14:06

Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa taasisi ya usilie tena wakitoa kadi ya bima ya afya kwatoto mwa mahitaji maalum, Picha na Hagai Ruyagila

Ebola ni ugonjwa hatari unaosababishwa na virusi vya Ebola na ugonjwa huu huenea kupitia kugusana na damu au majimaji ya mwili ya mtu aliyeambukizwa

Na Hagai Ruyagila

Wazazi na walezi wa watoto wenye mahitaji maalum wilayani Kasulu mkoani Kigoma wameaswa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola ili kuwakinga watoto wao na maambukizi ya ugonjwa huo.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, wakati akizungumza na wazazi na walezi wa watoto wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Buchuma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.

Kanali Mwakisu amesema ni muhimu kwa wazazi na walezi kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya kuhusu njia za kujikinga na ugonjwa wa Ebola, ikiwa ni pamoja na kudumisha usafi wa mazingira, kunawa mikono mara kwa mara na kutoa taarifa mapema wanapobaini dalili zinazohusishwa na ugonjwa huo.

Sauti ya Kanali Isaac Mwakisu

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Usilie Tena kutoka jijini Dar es Salaam amesema watoto wenye mahitaji maalum wana haki ya kupata elimu na huduma nyingine muhimu kama ilivyo kwa watoto wengine, hivyo jamii inapaswa kuendelea kuwapa uangalizi na msaada unaostahili.

Sauti ya Egla Kamugisha

Baadhi ya wazazi na walezi wilayani Kasulu wameiomba serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ugonjwa wa Ebola ili kuongeza uelewa wa wananchi na kusaidia kujikinga dhidi ya maambukizi.

Sauti ya Wazazi na walezi

Hata hivyo Serikali, taasisi mbalimbali na jamii kwa ujumla zimeendelea kushirikiana katika kutoa elimu ya afya na huduma kwa watoto wenye mahitaji maalum, huku wazazi na walezi wakihimizwa kuwa mstari wa mbele katika kulinda afya na ustawi wa watoto hao dhidi ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo Ebola.