Joy FM
Joy FM
1 June 2026, 13:20

Wauguzi ni nguzo muhimu katika mfumo wa afya na maendeleo ya taifa kwa sababu wanasaidia kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora na uwezo wa kushiriki katika shughuli za maendeleo
Na Emmanuel Kamangu
Wauguzi mkoani Kigoma wameaswa kuendelea kuzingatia maadili ya taaluma yao ili kuhakikisha wanatoa huduma bora za afya kwa wananchi, kwa kutanguliza huruma, upendo na utu kwa wagonjwa.
Wito huo umetolewa na Dkt. Damas Kayera kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Kijiji cha Makere. Amesema ni muhimu kwa wauguzi kuendeleza nidhamu na uwajibikaji kazini kwa manufaa ya wananchi wanaowahudumia.

Awali, Gidion Kipangula akisoma risala kwa niaba ya wauguzi mbele ya mgeni rasmi, alisema kuwa licha ya jitihada za serikali kuboresha maslahi yao, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazopunguza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akizungumzia changamoto hizo, Dkt. Kayera alisema serikali imeendelea kuajiri watumishi wa kada ya uuguzi na kuboresha maslahi yao. Kuhusu suala la sare za wauguzi, aliwataka wasimamizi wa sekta hiyo kuendelea kulifuatilia na kulisimamia kikamilifu ili kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa wa kuridhisha.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi walioshiriki maadhimisho hayo walitoa pongezi kwa wauguzi kwa mchango wao mkubwa katika utoaji wa huduma za afya. Mmoja wao, Penina Bernado, aliiomba serikali kuongeza idadi ya wauguzi na kuwajengea nyumba karibu na vituo vyao vya kazi ili kuwawezesha kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.
Naye Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Esta Kondo, aliwataka wauguzi kuenzi kwa vitendo mchango wa Florence Nightingale kwa kutoa huduma za afya kwa weledi, upendo na bila ubaguzi wa aina yoyote.