Joy FM
Joy FM
8 May 2026, 09:25

Mfumo huo unasaidia kufuatilia matumizi ya fedha, mapato na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa njia ya kidigitali, hivyo kuongeza uwazi na kupunguza makosa au upotevu wa fedha za umma
Na Mwandishi wetu
Wakuu wa Divisheni na Vitengo, pamoja na watendaji wengine wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, leo Jumatano Mei 6, 2026, wamepitishwa katika tathmini ya mafunzo ya Mfumo wa Ukaguzi wa Fedha (IFTMIS) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri wa Kagoma.
Katika mafunzo hayo, washiriki wametakiwa kutumia kwa ufanisi maarifa waliyopata hususan katika mchakato wa ujibuji wa hoja za ukaguzi, ambazo mara nyingi zimekuwa zikichafua taswira ya taasisi. Hivyo, wamehimizwa kuyapa kipaumbele mafunzo hayo ili kuimarisha uwajibikaji na kuondoa dosari zinazoweza kujitokeza.

Aidha, imeelekezwa kuwa kupitia mfumo wa IFTMIS, wakuu wa idara na vitengo sasa watakuwa na wajibu wa moja kwa moja wa kujibu hoja kupitia mfumo huo, tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo jukumu hilo lilitekelezwa zaidi na Mweka Hazina wa Halmashauri. Sambamba na hilo, washiriki wote wamehimizwa kufungua akaunti kwenye mfumo huo na kuutumia kikamilifu ili kuongeza ufanisi na uwazi katika usimamizi wa rasilimali za umma.
