Joy FM

Watumishi wakumbushwa matumizi sahihi ya mfumo wa PEPMIS Kasulu

15 July 2026, 16:58

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Kasulu, Nurfus Aziz Ndee, Picha na Hagai Ruyagila

Mfumo wa Upimaji wa Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma (PEPMIS) ni mfumo wa kidijitali unaotumika kuwasaidia watumishi wa umma kupanga, kutekeleza, kufuatilia na kutathmini utendaji wao wa kazi na mfumo huu umeanzishwa ili kuongeza uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi

Na Hagai Ruyagila

Watumishi wa Halmashauri ya Mji Kasulu wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya Mfumo wa Upimaji wa Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma (PEPMIS) katika utekelezaji wa mipango kazi ya mwaka pamoja na maandalizi ya mwaka mpya wa fedha 2026/2027.

Akizungumza katika kikao maalumu kilichowakutanisha watumishi wa halmashauri hiyo, Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Nduwayo Elias, amewasisitiza watumishi hao kuhakikisha wanaandaa na kuingiza taarifa kwenye mfumo kwa usahihi na kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa tathmini ya utendaji kazi.

Watumishi wa halmashauri wakipatiwa mafunzo ya mfumo wa upimaji wa utendaji kazi kwa watumishi wa umma PEMPMIS, Picha na Hagai Ruyagila

Aidha, amewasisitiza watumishi kuepuka kuingiza majukumu yanayojirudia katika mipango yao ya kazi, akieleza kuwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha kupungua kwa alama za tathmini ya utendaji kazi.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Nurfus Aziz Ndee, amewahimiza watumishi wote kuwasilisha changamoto wanazokutana nazo katika matumizi ya Mfumo wa PEPMIS kwa Ofisi ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati na kuhakikisha mfumo unatumika kwa ufanisi katika kuboresha utendaji wa watumishi.

Baadhi ya watumishi wameahidi kutumia mfumo huo kwa ufanisi sambamba na kutekeleza maelekezo yote waliyopewa

Mkuu wa Divisheni ya kutawala na usimamizi wa rasilimali watu halmashauri ya Mji Kasulu, Nduwayo Elias, Picha na Hagai Ruyagila