Joy FM

Wananchi watakiwa kudumisha amani na mshikamano Kigoma

7 July 2026, 11:32

Baadhi ya wananchi waliohudhuria msiba wa Kiongozi wa Kanisa la The New Hope Izenga, Picha na Sofia Cosmas

Amani ni msingi wa maendeleo ya taifa lolote duniani na bila amani hakuna maendeleo ya kudumu katika nyanja za uchumi, elimu, afya na ustawi wa jamii, hivyo kila mwananchi anapaswa kuitunza na kuilinda amani ili Tanzania iendelee kuwa taifa lenye umoja, usalama na maendeleo kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Na Sofia Cosmas

Wananchi Katika Manispaa ya Kigoma Ujiji wametakiwa kuendelea kuilinda amani ya Taifa letu kama walivyofanya waasisi wa taifa hili ambao walijitolea kwa nguvu na juhudi kuhakikisha nchi inapata uhuru na kudumisha umoja.

Wito huo umetolewa na Askofu Mkuu wa Makanisa ya The New Hope Tanzania na Mkurugenzi wa Cambridge Share, Askofu Josephati Chales Njige, wakati wa ibada maalumu ya kuuaga mwili wa marehemu Mchungaji Musa Fadhili Bernard wa Kanisa la The New Hope Izenga, wilayani Igunga mkoani Tabora.

Amesema jukumu la kuendelea kuilinda amani iliyopo ni la kila mtanzania bila kujali tofauti za kisiasa, dini au kabila.

Sauti ya Askofu Njige

Aidha, Askofu Njige amewashauri wananchi wa Mkoa wa Kigoma kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kubaini mapema magonjwa mbalimbali na kuanza matibabu kwa wakati na kujikinga na magonjwa hatari, ikiwemo homa ya ini, huku akisisitiza kuachana na dhana potofu kuhusu ugonjwa huo na badala yake kufuata ushauri wa madaktari.

Baadhi ya viongozi wa Kanisa akiwemo Bishop Njige, Picha na Sofia Cosmas

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliohudhuria ibada hiyo, akiwemo Vanisi Leonard kutoka Nkungwe na Fabian Josefu Nzigama, wamewataka Watanzania kuendelea kuilinda amani, umoja na mshikamano uliopo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Sauti za wananchi

Marehemu Mchungaji Musa Fadhili Bernard alizaliwa tarehe 26 Januari 1994 katika Kijiji cha Kalalangabo, Kata ya Ziwani, Mkoa wa Kigoma na amefariki dunia tarehe 3 Julai 2026, akiwa ameacha mjane mmoja na watoto wawili.

Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe. Amina.