Joy FM
Joy FM
17 June 2026, 21:24

Elimu ya kuchukua tahadhari ya mlipuko wa ebola imeendelea kutolewa kwa wananchi huku kukiwa hakuna taarifa za uwepo wa ugonjwa huo hapa nchini.
Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amesema mpaka sasa hakuna taarifa yoyote ya uwepo wa maradhi ya Ebola mkoani hapa huku akisisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Balozi Sirro amesema wataalam wa Afya wapo katika maeneo yote ya mipakani mwa Mkoa na nchi jirani ili kidhibiti uwezekano wa maradhi hayo kuenea mkoani hapa.
Amesema kwa sasa wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari dhidi ya wahamiaji haramu wanaoingia nchini kutoka nchi jirani bila kuzingatia taratibu za kisheria, jambo linaloweza kusababisha uwezekano wa kusambaa kwa maradhi hayo kwa wakazi wa Mkoa wa Kigoma.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Damas Kayera, amesema Mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, umeimarisha mifumo ya kukabiliana na ugonjwa huo katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na kuwajengea uwezo na utayari watumishi wa Idara ya hiyo.
Amesema kila kituo cha Afya katika Wilaya zote za Mkoa wa Kigoma kimewezeshwa vifaa kwa ajili ya kufanya uchunguzi na kutoa huduma za awali kwa atakayebainika kuwa na changamoto ya maradhi hayo, kabla ya kupelekwa katika kituo kikubwa cha huduma.
Dkt. Kayera ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa mara watakapobaini mtu yoyote mwenye viashiria vya ugonjwa huo katika vituo vya kutolea huduma za Afya vilivyopo jirani au kupiga simu namba 199.