Joy FM
Joy FM
13 July 2026, 16:06

Programu ya uongozi wa kitaaluma (Mentorship Programme) kwa waandishi wa habari wanawake ni hatua muhimu katika kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari nchini kwani waandishi wanapata nafasi ya kujifunza kutoka kwa wataalamu wenye uzoefu, jambo linalowawezesha kuongeza ujuzi, kujiamini na kuboresha utendaji wao wa kazi
Na Mwandis hi wetu
Waandishi wa habari wanawake kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wameanza rasmi programu ya uongozi wa kitaaluma (Mentorship Programme) inayotekelezwa na Media Council of Tanzania (MCT) kupitia mradi wa Media Rights, Equality and Inclusion (MREI) kwa ushirikiano na VIKES. Programu hiyo inalenga kuwawezesha waandishi hao kuimarisha uwezo wao wa kuzalisha habari zenye athari chanya kwa jamii, kuzingatia maadili ya taaluma na kukuza maendeleo yao ya kitaaluma.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo ya siku mbili yaliyofanyika katika Hoteli ya Seashells Millennium jijini Dar es Salaam, Katibu mtendaji wa baraza la Habari Tanzania Ernest Sungura amesema kuwa lengo la uandishi wa habari si kuripoti matukio pekee, bali kuzalisha habari zinazochochea mjadala wa maendeleo, zinahamasisha uwajibikaji na kuibua suluhisho la changamoto zinazoikabili jamii.

“Jiulizeni kila mara, lengo la stori yenu ni nini? Kama habari haiwezi kuleta mabadiliko, kuhamasisha hatua au kuchochea mjadala wa maendeleo, basi bado kuna nafasi ya kuiboresha,” alisema.
Aliongeza kuwa waandishi wa habari wanapaswa kuelekeza nguvu zao katika kuandika habari zinazogusa maisha ya wananchi wa kawaida na zinazochangia mabadiliko chanya, badala ya kuandika kwa ajili ya kuripoti matukio bila kuangalia athari zake kwa jamii.
Katika mafunzo hayo, washiriki walijifunza umuhimu wa uhusiano wa kitaaluma kati ya mentor na mentee, maadili ya uandishi wa habari, namna ya kuandaa story pitches zenye athari, pamoja na kuweka malengo ya maendeleo ya taaluma zao.

Programu hiyo ya mentorship itatekelezwa kwa kipindi cha miezi sita, ambapo washiriki watapata mwongozo na ushauri kutoka kwa waandishi wa habari wenye uzoefu ili kuwawezesha kuzalisha habari zenye athari (Impact Journalism) zinazochochea uwajibikaji na maendeleo ya jamii.
Mradi huu ni sehemu ya juhudi la Baraza la habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na VIKES za kuimarisha ushiriki wa wanawake katika sekta ya habari, kukuza uongozi wao ndani ya vyombo vya habari na kuongeza uzalishaji wa habari zinazozingatia usawa, ujumuishi na maslahi ya umma.