Joy FM
Joy FM
27 July 2026, 11:24

Usafi wa mazingira ni jambo muhimu katika maisha ya kila siku na mazingira safi huchangia afya bora ya watu, huongeza ustawi wa jamii, na husaidia kuzuia kuenea kwa magonjwa
Na Hagai Ruyagila
Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kuzingatia usafi wa mazingira katika makazi na maeneo yao ya biashara ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira.
Wito huo umetolewa na Kaimu wa Kitengo cha Usafi na Udhibiti wa Taka wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Malagera Lukiko, wakati wa zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika katika eneo la Mnarani, Kata ya Kumnyika, ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.

Lukiko amesema mazingira machafu ni chanzo kikuu cha kuenea kwa magonjwa ya mlipuko, hivyo amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za usafi na kuhakikisha maeneo ya makazi pamoja na biashara yanakuwa safi wakati wote.
Pia amesema endapo mwananchi yeyote atapinga kushiriki katika zoezi hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwinyi, Silvanicatus William, amesema zoezi hilo ni muhimu katika kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko.

Aidha, amewataka wananchi kuhakikisha wanakuwa na ndoo za kunawia mikono katika maeneo yao ili kuendelea kudumisha afya na kuzuia maambukizi ya magonjwa.
Baadhi ya wananchi ~walioshiriki katika zoezi hilo wamesema kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kuhusu usafi wa mazingira ili kuongeza uelewa na hamasa ya wananchi kushiriki katika shughuli za usafi, hatua ambayo itachangia kuboresha afya na ustawi wa jamii.