Joy FM

RC Sirro aalika wawekezaji Burundi, Congo kuwekeza Kigoma

23 September 2026, 12:06

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro, Picha na Mwandishi wetu

Mazingira wezeshi na miundombinu inayoendelea kuwekwa na serikali imesaidia Mkoa wa Kigoma kuendelea kuwa kitovu cha biashara kwa nchi zinazozunguka ziwa Tanganyika

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro, ametoa wito kwa wafanyabiashara kutoka nchi jirani za Congo DR na Burundi kuwekeza mkoani hapa kutokana na uwepo fursa nyingi za uwekezaji katika Sekta za viwanda, biashara, Uchukuzi, Kilimo, Uvuvi na Utalii.

Balozi Sirro ametoa wito huo alipofunga rasmi maonesho ya biashara ya Lake Tanganyika International Expro 2026, yaliyofanyika Manispaa ya Kigoma Ujiji na kuwakutanisha wafanyabiashara kutoka nchi za Burundi, Congo DR na kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Amesema maonesho hayo yameonesha mafanikio kwa kuunganisha wazalishaji wa bidhaa na masoko pamoja na kuvutia wawekezaji na wabia wa Maendeleo sambamba na kuhamasisha matumizi ya teknolojia, kuibua ubinifu na kukuza biashara, ajira na uchumi wa wananchi.

Aidha, Sirro amesisitiza kuwa, maonesho hayo yanalenga kuimarisha diplomasia ya uchumi katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika kwa lengo la kukuza uchumi wa mataifa hayo kupitia mafanikio ya mtu mmoja mmoja au taasisi.

Naye Waziri wa Madini Mkoa wa Tanganyika nchini Congo DR Mateka Simplis, amesema uhusiano unaozidi kuimarika katika sekta ya biashara baina ya nchi ya Congo DR na Tanzania, unatoa fursa muhimu ya kuzifungua pande mbili hizo kiuchumi.

Amesema nchi hiyo imekuwa ikitegemea bidhaa nyingi kutoka Tanzania ambapo amewasisitiza wafanyabiashara nchini kuendelea kushirikiana kwa karibu na wenzao wa Congo ili kurahisisha upatikanaji wa masoko kwa pande zote mbili.

Upande wake mwakilishi wa Balozi katika ubalozi mdogo wa Congo DR,Adalbert Nininahazwe amesema maonesho ya Lake Tanganyika International Expro 2026 yanapaswa kuwa endelevu huku yakionesha mashirikiano makubwa ya kiuchumi na kimahusiano yaliyopo baina ya nchi Shiriki.

Maonesho ya Lake Tanganyika International Expo 2026, yameandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwa kushirikiana na Chemba ya wafanyabiashara(TNCC) na kudhaminiwa na Program ya Pamoja ya Kigoma (KJP), Shirika la Enable pamoja na Mati Super Brand Co. Ltd.