Joy FM
Joy FM
17 November 2026, 16:59

Mwanafunzi anahitaji kuchagua fani au masomo yatakayomsaidia kufikia malengo yake ya baadaye na uchaguzi huu unahitaji ushirikiano kati ya wazazi, walimu na mwanafunzi mwenyewe ili kufanya uamuzi sahihi.
Na Mwandishi wetu
Wazazi na Walimu Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma, wametakiwa kushirikiana na watoto wao na kuwatia
moyo wa kuendelea na masomo na kuchagua fani wanazozipenda ili waweze kuzifikia fursa mbali mbali
zilizoko mbele yao.
Hayo yameelezwa na afisa kutoka Shirika la Maendeleo la Ubelgiji ENABEL, anayeshughulikia masuala ya
elimu, Haji Vuai Haji, wakati wanafunzi zaidi ya 300 kutoka shule za sekondari wilayani Kasulu,
walipofanya ziara katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi FDC, kwa ajili ya mafunzo ya fursa za ajira na
kujiajiri.

Ziara hiyo iliyoratibiwa na ENABEL kupitia mradi wa ‘Wezesha Binti’ imelenga kuwaonyesha wanafunzi
hao fursa za ajira na kujiajiri kupitia ujuzi unaotolewa katika chuo hicho, ili waweze kuchagua fani
wanazozipenda wakati wakiendelea na masomo yao, na hapa baadhi ya wanafunzi wanaeleza.
Kwa upande wake Faraja James, ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Mji Kasulu,
amesema mradi wa Wezesha Binti, umekuwa na tija na kwamba serikali inalenga kuendeleza yote
yanayofanywa kupitia mradi huo pindi utakapofika mwisho ifikapo mwaka 2027.
Mradi wa ‘Wezesha Binti’ unalenga kuwawezesha vijana wenye umri wa kati miaka 14 na 29 ambapo
pamoja na mambo mengine, unaboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu bora na mafunzo ya amali.