Joy FM
Joy FM
17 November 2026, 17:34

Wananchi Wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma wametakiwa kulima mazao ya kimkakati
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, Mhe. Festo Kiswaga, amewataka wananchi wilayani humo kuchangamkia fursa ya kulima mazao ya kimkakati yenye tija na soko la uhakika kama vile choroko, mbaazi, tumbaku, kahawa na parachichi.
Amesema kuwa mazao hayo yana uwezo mkubwa wa kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja na kukuza uchumi wa wilaya kwa ujumla.

Kiswaga ameyasema hayo wakati wa ziara ya kikazi katika kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe kwa lengo la kujitambulisha rasmi kwa wananchi, kusikiliza kero zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi wa haraka.
Mbali na utatuzi wa kero, DC ametumia mikutano hiyo ya hadhara kuwasilisha ajenda za maendeleo, hususan kuhamasisha wananchi kubadilika na kujikita katika kilimo biashara badala ya kilimo cha kujikimu pekee.

Kwa upande wao, wananchi wa kata hizo wameipongeza hatua hiyo ya kiongozi wao kuwafuata katika maeneo yao, wakieleza kuwa inawapa fursa ya kueleza changamoto zao moja kwa moja na kupata mwanga mpya kuhusu fursa za kiuchumi zinazowazunguka.