Joy FM
Joy FM
27 October 2026, 15:01

Vijana kuunda vikundi ili kutambulika kunasaidia serikali kuweza kupata takwimu na orodha ya vikundi vyao na namna ya kuwawezesha kupitia programu mbalimbali
Na Hagai Ruyagila
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Theresia Mtelewe, amewataka vijana kutoka wilaya za Kasulu na kibondo mkoani Kigoma kujiunga na vikundi vinavyotambulika na serikali ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na serikali kupitia halmashauri na kujikwamua kiuchumi.
Mtelewe ametoa wito huo wakati akizungumza na vijana 150 wa wilaya hizo katika ukumbi wa Dubai Plaza uliopo mjini Kasulu, akieleza kuwa mikopo hiyo ni miongoni mwa fursa zinazolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Amesema mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na halmashauri kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu haina riba, huku akiwataka wanufaika kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuongeza nafasi ya kupata mikopo mikubwa zaidi siku zijazo.
Aidha, Mtelewe amesema serikali imeweka fedha katika benki mbalimbali nchini kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kupata mikopo yenye riba nafuu, akiwataka vijana wenye mitaji na mipango mizuri ya biashara kutumia fursa hiyo kuanzisha na kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Pelimina Msuta, ameeleza baadhi ya sifa zinazotakiwa ili kijana aweze kunufaika na mikopo hiyo, ikiwemo kuwa raia wa Tanzania.
Baadhi ya vijana kutoka katika wilaya za Kibondo na Kasulu wameeleza maoni yao kuhusu fursa za mikopo na namna zinavyoweza kuwasaidia kuboresha shughuli zao za kiuchumi.