Joy FM
Joy FM
12 October 2026, 21:51

Watoto wa kike wanapaswa kuchukua tahadhari ikiwemo kuepuka vishawishi ili kulinda utu wao na kutoa taarifa wanapobaini viashiria vya kutendewa uovu vinavyosababisha kukiukwa kwa haki zao
Na Mwandishi wetu
Katika kuadhimisha Kilele cha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, Mkoa wa Kigoma umeungana na mataifa mengine kuadhimisha siku hii muhimu kwa ajili ya kutambua haki za watoto wa kike ili kuendelea kuangazia changamoto za kipekee zinazolikabili kundi hilo.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na uwepo kwa mfumo dume, mila na desturi kandamizi, pamoja na umasikini unaoendelea kurejesha nyuma ustawi wa mtoto wa kike kupata haki na kufikia malengo.

Akichangia mada kwenye kongamano fupi lililokwenda sambamba na kilele cha maadhimisho hayo kimkoa, kilichofanyika Shule ya Msingi Gungu katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, Zaina Yahaya Mwanafunzi wa Shule hiyo, amesema jamii inapaswa kuzitambua na kuzitekeleza kwa vitendo haki za kundi hilo.

Upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Kigoma Msafiri Nzunuri, amesema wazazi wanapaswa kuongeza ushiriki wa watoto wa kike katika maamuzi na kufanyia kazi ushauri wao kuhusu masuala yanayowagusa.
“Wazazi wanapaswa kupunguza ukali na kutumia muda wao kuzungumza na watoto bila kuona aibu ili kupata taarifa za masuala mbalimbali yanayotendeka dhidi yao nyumbani, shuleni au katika jamii wanayoishi” amesema Nzunuri.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Rehema Nduka ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii, ametoa wito wa kuhakikisha watoto wa kike wanapata fursa za kunufaika na rasilimali za nchi kama vile ardhi, elimu ya juu, ajira, mikopo ya biashara na haki nyingine za Msingi za binadamu.Aidha amewataka wazazi kutoa huduma za Msingi ikiwemo kuwawezesha watoto wa kike kufika shuleni kwa usalama sambamba na kupata chakula kabla au wawapo shuleni ili kuwapunguzia adha ya kushinda bila kula.
Akimwakilisha Katibu Tawala Mkoa, Afisa Elimu ya Watu Wazima Mkoa wa Kigoma, Mwalimu Fausta Akaro amesema mila na desturi bado zimebaki kuwa kikwazo kikubwa kwa makuzi na maendeleo ya mtoto wa kike.
“Natoa wito kwa wazazi kuhakikisha watoto wa kike wanatazamwa kwa usawa kama watoto wa kiume, nao wapewe nafasi ya kucheza, kujifunza, kujenga urafiki salama na kushiriki katika mambo yanayowahusu ili wakue kimwili, kiakili na kijamii” amesema Akaro.
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike duniani 2026, yanakauli mbinu isemayo “Wekeza kwa Mtoto wa Kike: Tokomeza Ndoa za Utotoni.