Joy FM
Joy FM
12 October 2026, 12:29

Mwalimu ni mtu muhimu katika jamii kwa sababu ana jukumu la kufundisha, kulea na kuwaongoza wanafunzi katika kupata maarifa, ujuzi na tabia njema hivyo maadili ni msingi mkubwa wa kusaidia kumjenga mwanafunzi
Na Hagai Ruyagila
Walimu wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma, wametakiwa kuzingatia maadili ya kazi na kuwa waadilifu wanapotekeleza majukumu yao ya ufundishaji ili kulinda haki, usalama na mustakabali wa wanafunzi.
Wito huo umetolewa na Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Kigoma, Mwl. Tumaini Daniel, wakati akizungumza na walimu wa Shule ya Sekondari Bogwe iliyopo Halmashauri ya Mji Kasulu, katika ziara yake ya siku moja shuleni hapo.
Amesema baadhi ya walimu wamekuwa wakikiuka maadili ya taaluma hiyo kwa kuwashawishi wanafunzi kushiriki nao katika vitendo vya kingono, jambo alilolieleza kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa maadili na linaweza kuathiri maisha ya wanafunzi pamoja na hadhi ya taaluma ya ualimu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Kasulu, Mwl. Elisha Kebelo, amesema chama hicho kinaendelea kuhimiza walimu kuzingatia maadili ya taaluma, kuwa waadilifu na kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kuboresha utoaji wa elimu.

Baadhi ya walimu katika Halmashauri ya Mji Kasulu wamesema vitendo vya ukiukwaji wa maadili miongoni mwa baadhi ya walimu vinatokana na kutofuata misingi na taratibu za taaluma, huku wakisisitiza umuhimu wa kila mwalimu kuwajibika na kuwa mfano bora kwa wanafunzi.
Kwa ujumla, walimu wametakiwa kuzingatia maadili ya taaluma, kulinda haki na usalama wa wanafunzi, pamoja na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu ili kujenga mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji.