Joy FM

Vyama 11 vya upinzani vyaunga mkono Ndayishimiye uchaguzi wa 2027 Burundi

11 November 2026, 10:43

Baadhi ya wanachama wa vyama upinzani, picha na Bukuru Daniel

Uchaguzi wa Urais nchini Burundi unatarajiwa kufanyika mei 3, mwaka 2027

Na Bukuru Daniel

Vyama 11 vya upinzani nchini Burundi vimetangaza kumuunga mkono Rais Évariste Ndayishimiye katika azma yake ya kuwania muhula wa pili wa urais, katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Mei 3 mwaka 2027.

Uamuzi huo ulitangazwa Jumanne mjini Bujumbura, ambapo vyama hivyo vilieleza kuwa vimekubaliana kuungana na kuendesha kampeni ya pamoja kumuunga mkono mgombea wa chama tawala cha CNDD-FDD.

Baadhi ya viongozi wa vyama vya upindazano wakiwa kwenye mkutano

Katika taarifa yao ya pamoja, vyama hivyo, vikiwemo FROLINA, KAZE-FDD na RADEBU, vimesema vimezingatia juhudi za Rais Ndayishimiye katika kupambana na rushwa, kulinda mamlaka ya taifa na kudumisha usalama wa raia na mali zao.

Aidha, vimeahidi kutoa mchango wao katika utekelezaji wa dira ya taifa na kujenga nchi inayozingatia utawala wa sheria, uhuru na haki kwa wote.

Wanachama wa vyama vya upinzani wakiwa katika mkutano, Picha na Bukuru Daniel

Kwa mujibu wa ratiba ya tume huru ya taifa ya uchaguzi, wagombea urais wanapaswa kuwasilisha nyaraka za kugombea kati ya Novemba 13 na 22 mwaka huu.

Rais Evariste Ndayishimiye, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2020, aliteuliwa na chama cha CNDD-FDD mwezi Aprili kuwa mgombea wake katika uchaguzi huo.