Joy FM

TARURA yatakiwa kusimamia matumizi ya barabara Kasulu

13 November 2026, 18:03

Madiwa katika halmashauri ya Mji wa Kasulu wakiwa katika kikao, Picha na Hagai Ruyagila

Matumizi mabaya ya barabara yameendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali hali inayosababisha barabara nyingi kuharibika na kushindwa kupitika

Na Hagai Ruyagila

Madiwani Katika Halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani kigoma wameitaka TARURA wilaya ya Kasulu kuhakikisha wanasimamia sheria na taratibu za matumizi ya barabara ili magari yanayoruhusiwa kupita yanaendana na uzito unaoruhusiwa kwa kila barabara, ili ziweze kudumu kwa muda mrefu.

Madiwa wa Halmashauri ya Mji wa kasulu, Picha na Hagai Ruyagila

Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri ya Mji Kasulu robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, kipindi cha Julai hadi Septemba Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mh. Ayubu Ngalaba amesema baadhi ya madereva wamekuwa wakitumia barabara bila kuzingatia uzito wa magari yanayoruhusiwa kupita katika barabara husika, hali inayochangia uharibifu wa miundombinu hiyo na kuongeza gharama za matengenezo.

Amesema TARURA inapaswa kusimamia changamoto hiyo na kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya madereva watakao kiuka Sheria za usalama barabarani hususan kwa kutumia barabara za magari madogo.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mh. Ayubu Ngalaba, Picha na Hagai Ruyagila

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TARURA wilaya ya Kasulu, Mhandisi Erick Laban, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa taasisi hiyo itafanyia kazi suala hilo kwa kuhakikisha wanasimamia ipasavyo sheria na taratibu zilizopo.

Kaimu Meneja wa TARURA wilaya ya Kasulu, Mhandisi Erick Laban, Picha na Hagai Ruyagila

Katibu wa Chama Cha Wananchi CUF wilaya ya Kasulu Ahmad Dugala amesema lengo la kutii sheria lina tija katika kutunza miundombinu ya barabara ili usalama uendelee kuwepo katika barabara za Mji wa Kasulu.