Joy FM
Joy FM
30 June 2026, 09:03

Ardhi ni rasilimali muhimu inayochangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla kupitia matumizi bora ya ardhi, shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile kilimo, ufugaji, makazi na uwekezaji hupangwa kwa ufanisi, jambo linalosaidia kuongeza uzalishaji, kulinda mazingira na kudumisha amani miongoni mwa wananchi
Na Mwandishi wetu
Mkurugenzi Mtendaji amekutana na wajumbe wa Serikali za Vijiji, afisa kilimo na mifugo, watendaji wa Vijiji na kata na Waheshimiwa Madiwani kutoka kata ya Kasanda na Kiziguzigu kwa lengo la kupitia mpango wa matumizi bora ya ardhi unaohusisha kutenga maeneo ya malisho kwa ajili ya wafugaji na eneo la kilimo.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika leo Jumatatu Juni 29, 2026 katika ukumbi mpya wa halmashauri, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndaki Stephano Mhuli amewasisitiza wajumbe wa Serikali za Vijiji kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za matumizi ya ardhi huku akisisitiza kutatua migogoro ya ardhi kwa makubaliano bila kuchukua sheria mkononi.

Mbunge wa Jimbo la Kakonko, Mhe.Allan Mvano ameeleza kuwa hakuna sababu ya wakulima na wafugaji kuwa na migogoro ya ardhi badala yake makundi hayo yashirikiane kwa pamoja ili kujenga mshikamano na upendo hatimaye kuleta tija katika uzalishaji mali.
Afisa Ardhi wa Wilaya, Gideon Kimaro, ameeleza kuwa Halmashauri imepanga matumizi bora ya ardhi kwa kubainisha na kutenga ardhi kwa ajili ya kilimo na eneo kwa ajili ya ufugaji ili kuepuka muingiliano kati ya wakulima na wafugaji hivyo ni muhimu pande hizo mbili kuzingatia sheria taratibu na kanuni za matumizi bora ya ardhi.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kasanda, Thomas Peter Gwamikiko, amishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kupanga matumizi bora ya Ardhi kwa ajili ya wakulima na wafugaji hivyo ameahidi kwenda kuwaelimisha Wananchi kuhusiana na matumizi bora ya ardhi.