Joy FM

Moto wateketeza vibanda tisa soko la Muganza Kasulu

11 July 2026, 12:13

Muonekano wa sehemu ya vibanda tisa vilivyoteketea kwa moto Soko la Muganza, Picha na Hagai Ruyagila

Wananchi na wafanyabiashara katika masoko mbalimbali yaliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kuchukua tahadhali ya moto wawapo katika shughuli zao za kila siku ili kuepuka kuwa chanzo cha majanga ya moto

Na Hagai Ruyagila

Zaidi ya vibanda tisa katika Soko la Muganza, lililopo Kata ya Mganza, Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma, vimeteketea kwa moto kufuatia ajali inayodaiwa kusababishwa na mafuta ya mawese yaliyokuwa yakichemshwa na mmoja wa wafanyabiashara sokoni hapo.

Baadhi ya wananchi wa eneo la Muganza wakiwa katika eneo la tukio la moto ulioteketeza vibanda, Picha na Hagai Ruyagila

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, lililotokea leo Julai 10, 2026, katika soko la Muganza wamesema mfanyabiashara huyo alidaiwa kuchemsha mafuta ya mawese ndani ya kibanda chake, kisha kufunga mlango na kuondoka huku mafuta yakiendelea kuchemka. Hali hiyo inadaiwa kusababisha moto ulioenea kwa kasi na kuteketeza vibanda hivyo pamoja na mali mbalimbali za wafanyabiashara.

Akizungumza baada ya kutembelea eneo la tukio, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwalimu Vumilia Julius Simbeye, amewapa pole wafanyabiashara waliopata hasara kutokana na janga hilo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu Mwal. Vumilia Simbeye, Picha na Hagai Ruyagila

Aidha Mwl, Simbeye amewashauri wafanya biashara hao kujenga vibanda kwa kutumia matofali na vifaa vinavyostahimili moto ili kupunguza athari za namna hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, amemtaka mtu anayehusishwa na chanzo cha moto huo kujisalimisha katika Kituo cha Polisi kwa ajili ya uchunguzi na hatua za kisheria. Amesisitiza kuwa uzembe unaohatarisha maisha na mali za wananchi hautavumiliwa.

Mkuu wa Wilaya Kasulu Kanali Isac Mwakisu akizungumza na wananchi mara baada ya kutembelea eneo la tukio la vibanda vilivyoteketea kwa moto, Picha na Hagai Ruyagila

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Wananchi wamefanikiwa kuudhibiti moto huo na kuzuia usienee katika maeneo mengine ya soko, huku tathmini ya kina ya hasara iliyosababishwa ikiendelea kufanywa.

Baadhi ya wafanyabiashara ambao vibanda vyao vimeteketea kwa moto, Picha na Hagai Ruyagila