Joy FM
Joy FM
9 June 2026, 11:22

Mikopo hiyo inayotolewa na Benki ya CRDB ambayo inatokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ni moja ya njia muhimu za kuwawezesha wananchi wenye kipato cha kujikwamua kiuchumi na mikopo hii imeanzishwa kwa lengo la kuwapa wanufaika mtaji wa kuanzisha au kuendeleza shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na hivyo kuboresha maisha yao na ya familia zao
Na Lucas Hoha
Wanufaika wa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 300 katika Manispaa ya Kigoma Ujiji wametakiwa kutumia fedha hizo kwa bidii, weledi wa ujasiriamali na usimamizi mzuri wa biashara zao ili kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati na kuepuka hatua za kisheria zitakazoweza kuchukuliwa dhidi yao.
Taarifa na Lucas Hoha.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji ambaye pia ni Afisa Elimu Sekondari wa manispaa hiyo, Kajanja Lawi, wakati akifungua mafunzo kwa vikundi 30 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilivyonufaika na mikopo hiyo.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Jabir Majira, amesema manispaa hiyo inaendelea kutekeleza sera, kanuni na miongozo ya Serikali kwa kuhakikisha mikopo hiyo inatolewa kwa wakati, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wananchi kiuchumi na kupunguza umasikini.
Nao baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa mikopo kwa wajasiriamali, wakisema hatua hiyo imewasaidia kuongeza uzalishaji na kuendesha shughuli zao za kiuchumi kwa ufanisi zaidi.
Mikopo hiyo imetolewa kwa vikundi mbalimbali vya wajasiriamali katika Manispaa ya Kigoma Ujiji kupitia Benki ya CRDB Tawi la Kigoma, kwa mujibu wa maelekezo na miongozo ya Serikali.