Joy FM
Joy FM
30 July 2026, 09:33

Wafanyabiashara wadogo wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji wametakiwa kutumia vyema fursa za kiuchumi wanazopewa ili kujikwamua kiuchumi na kujipatia maendeleo endelevu kwa ustawi wa jamii ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuwapatia vifaa wezeshi kwa ajili ya shughili zao za kila siku.
Na Sadick Kibwana
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Mashirika yasiyo ya kiserikali Manispaa ya Kigoma Ujiji, Bi. Thabitha Everist Mkilamweni amesema hayo wakati akizungumza katika hafla ya ugawaji wa vifaa kwa wafanyabiashara wadogo iliyoandaliwa na Taasisi ya Clear Vision For Change – CIVISCE, kwa kushirikiana na Women in Africa Venturing Education – WAVE.

Bi. Mkilamweni amesema fursa hizo zimetolewa kwa lengo la kuwainua wanawake wajasiriamali, hivyo wanapaswa kuzitumia kwa ufanisi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake Alexia Kiloga Mjumbe wa Baraza la Uratibu wa Mashirika yasiyo ya kiserikali Tanzania Bara Mkoa wa Kigoma amesema kazi ya mashirika ni kufika sehemu ambayo serikali imechelewa kufika na dhamira ikiwa wananchi wanaishi kwa usawa.
Naye, Meneja Mradi wa Taasisi ya CIVISCE, Bw. Mapendano B. Nabulizi, amesema vifaa hivyo vimetolewa kama mtaji wa kuanzia ili kuwawezesha kiuchumi wanawake hao.
Baadhi ya wafanyabiashara walionufaika wamesema elimu waliyoipata pamoja na vifaa hivyo vitawasaidia kupanua na kukuza biashara zao.
Awali, Taasisi ya Clear Vision for Change ilitoa mafunzo ya siku 5 kwa wafanyabiashara hao, yaliyolenga kuwajengea uwezo wa usimamizi wa fedha na ujasiriamali, kisha ikawagawia vifaa ikiwemo Incubator, friza, na maderi ya kuhifadhia samaki.