Joy FM
Joy FM
17 September 2026, 12:30

Chanjo ya wanyama ni muhimu sana katika ufugaji kwa sababu husaidia kuzuia magonjwa mbalimbali yanayoweza kuathiri wanyama kama ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku na mbwa wanaweza kushambuliwa na magonjwa ambayo yanaweza kusababisha vifo na hasara kubwa kwa wafugaji
Na Hagai Ruyagila
Wananchi na wafugaji katika Halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kuhakikisha mifugo yao, hususan mbuzi na kondoo, inachanjwa dhidi ya ugonjwa wa sotoka kuelekea kipindi cha masika.
Wito huo umetolewa na Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Mji Kasulu ambaye pia ni Mratibu wa Chanjo, Mariot Paul Chikwela, wakati wa zoezi la utoaji chanjo kwa mifugo katika maeneo mbalimbali ya halmashauri hiyo.

Chikwela amesema halmashauri imejipanga kuendelea kudhibiti magonjwa ya mifugo yanayosababishwa na virusi kwa kutumia chanjo pamoja na kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu kinga na udhibiti wa magonjwa hayo.
Amesema chanjo hiyo inatolewa kwa ruzuku ya nusu bei, ambapo mfugaji anachanja mbuzi au kondoo mmoja kwa shilingi 300 badala ya shilingi 700, hatua inayolenga kuwawezesha wafugaji wengi zaidi kupata huduma hiyo.

Aidha, Chikwela amebainisha dalili za ugonjwa huo kwa mbuzi na kondoo ikiwemo mafua makali na kuharisha.
Kwa upande wao, wafugaji walioshiriki katika zoezi hilo wameishukuru Serikali kwa hatua hiyo, huku wakiomba kuendelea kupewa elimu na semina kuhusu magonjwa ya mifugo, njia za kuyazuia pamoja na namna bora ya kuyadhibiti.
Zoezi hilo limefanyika katika Kata za Kigondo, Ruhita, Nyumbigwa, Murufiti na Nyasha, kufuatia kuibuka kwa ugonjwa wa sotoka katika maeneo hayo mwishoni mwa mwezi Mei mwaka 2026.