Joy FM
Joy FM
21 April 2026, 09:32

Wanafunzi wa Kidato cha sita, katika shule ya sekondari Kigoma Grand, halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma, wametakiwa kuendeleza nidhamu waliyopata shuleni hapo ili wawe mfano wa kuigwa katika jamii inayowazunguka.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kasulu Mwl. Vumilia Simbeye akiwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya saba ya kidato cha sita yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Samia Hall uliopo shuleni hapo.

Mwl. Simbeye amewasisitiza wanafunzi hao kuendeleza nidhamu waliyojifunza shuleni, akieleza kuwa malezi bora waliyopewa yanapaswa kuwa msingi wa mwenendo wao katika maisha yao ya baadaye na kuwafanya kuwa mfano mzuri kwa jamii.
Baadhi wanafunzi hao wa kidato cha sita ambao wanatarajia kuhitimu masomo yao hivi karibuni, wameeleza kuwa wataendelea kuzingatia maadili na nidhamu waliyojifunza shuleni ili kufikia malengo yao na kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Jumla ya wanafunzi 142 wa kidato cha sita wanatarajia kuhitimu masomo yao mwezi mei mwaka huu katika shule ya sekondari Kigoma Grand iliyopo Mjini Kasulu.