Joy FM

Kambi ya wakimbizi Nduta Kibondo imefungwa rasmi

1 May 2026, 09:49

Baadhi ya viongozi wakiwa katika hafla ya ufungaji wa kambi ya wakimbizi Nduta Kibondo, Picha na Mwandishi wetu

Serikali imefunga rasimi Kambi iliyokuwa inahifadhi wakimbizi kutoka Nchini Burundi Nduta, iliyoko Wilayani Kibondo Mkoani Kigoma, ikiwa ni baada ya Wakimbizi kulejea katika Nchi yao ya asili kwa hiyari na kuungana na ndugu zao.

Na Mwandishi wetu

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Patrobas Katambi amefunga rasmi Kambi ya wakimbizi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo mkoani hapa.

Kambi hiyo ilikuwa imehifadhi zaidi ya wakimbizi laki moja kutoka nchini Burundi ambao kwa sasa wamerejeswa kwenye nchi yao kufuatia hali ya amani na utulivu kutengemaa.

Kupitia Hotuba yake, Katambi amewataka watanzania kutathmini athari za  maisha ya ukimbizi jambo litakalowafanya waendelee kulinda amani ya nchi.

Sauti ya mwandishi wetu Kadislaus Ezekiel

Aidha, amesema Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Burundi pamoja na Mashirika ya kimataifa, wamefanikiwa kuwarejesha  jumla ya wakimbizi 165,494 kwa hali ya amani na utulivu.

Waziri Katambi akiwa na Mkuu wa Mkoa Kigoma na baadhiya viongozi baada ya kuwasili katika hafla ya kufunga kambi ya Nduta, Picha na Mwandishi wetu

Ameyashukuru mashirika yote yaliyokuwa yakitekeleza majukumu yao chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), kwa mchango wao mkubwa tangu kuanzishwa kwa kambi hiyo mpaka kufungwa.

Pia ameushukuru uongozi wa mkoa pamoja na wakazi wa Wilaya ya Kibondo kwa kuridhia maeneo yao kutumika kwa ajili ya makazi ya wakimbizi sambamba na kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza kutokana na uwepo wa wakimbizi hao.

Kwa sasa Mkoa wa Kigoma umebakiwa na kambi moja ya wakimbizi ya Nyarugusu iliyopo Wilayani Kasulu ambapo serikali inaendelea na zoezi la urejeshaji ili iweze kufunga eneo la wakimbizi kutoka nchini Burundi.

Muonekano wa jengo katika kambi ya wakimbizi Nduta iliyofungwa rasmi, Picha na Mwandishi wetu