Joy FM
Joy FM
14 May 2026, 16:04

Ukosefu wa maji huathiri shughuli za kiuchumi za wananchi na hushindwa kufanya shughuli zao kwa ufanisi kutokana na upungufu wa maji
Na Mwandishi wetu
Wananchi wa Kijiji cha Kasuku Kata ya Simbo Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wamelalamikia ukosefu wa huduma ya maji katika kijiji chao hali ambayo inawaathiri pakubwa katika shughuli zote zinazohitaji huduma hiyo muhimu.
Wametoa malalamiko hayo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua kwenye mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi, uliofanyika jana katika kijiji cha Kasuku, ambapo suala la maji liliibuka kuwa moja ya changamoto kubwa inayowakabili wakazi wa kijiji hicho.

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho akiwemo Mpoma Hamimu Mpoma, wamesema licha ya kuahidiwa kuchimbiwa visima katika kijiji chao na kijiji jirani cha Machazo,takribani miaka mitatu iliyopita, lakini majirani zao wanapata maji huku kijiji chao kikiwa hakina huduma hiyo muhimu.
Kufuatia malalamiko hayo Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua, akamtaka Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini RUWASA, Wilaya ya Kigoma Bwana Yesaya Kyungu, kusimama na kutoa maelezo kwa wananchi wa kijiji cha Kasuku kuhusu huduma ya maji kijijin hapo.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashd Chuachua, alilazimika kuahirisha mkutano huo kutokana na giza kuingia huku akiahidi kurejea kijijini hapo kwa ajili ya kukamilisha zoezi la kusikiliza kero za wananchi wa kijiji hicho na kuzitafutia ufumbuzi.