Joy FM

Bilioni 3.2 zakusanywa kwa mwaka wa Fedha 2025/2026 Kasulu

12 May 2026, 16:16

Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Kasulu Mwl. Vumilia Simbeye akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kasulu, Picha na Hagai Ruyagila

Mapato yanasaidia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa miundombinu, utoaji wa huduma za kijamii, pamoja na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wananchi

Na Hagai Ryagila

Halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 3.2 za mapato ya ndani kuanzia mwezi Julai hadi Mei 07 katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwl. Vumilia Simbeye, wakati akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake Mjini Kasulu.

Amesema kuanzia mwezi Januari hadi Machi mwaka huu, halmashauri hiyo imekusanya zaidi ya shilingi milioni 800, hali inayoonyesha uwezekano mkubwa wa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo hadi sasa wamefanikiwa kufikia asilimia 86 ya lengo walilijiwekea.

Sauti ya Mkurugenzi Kasulu Mji Kasulu

Aidha Mwl. Simbeye amesema mikakati mbali mbali iliyowekwa itasaidia kuongeza mapato na kufanikisha kuvuka lengo hilo.

Sauti ya Mkurugenzi Kasulu Mji Kasulu

Hata hivyo amebainisha kuwa tangu ateuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuiongoza halmashauri hiyo, Halmashauri ya Mji Kasulu imekuwa ikivuka lengo ya ukusanyaji wa mapato kila mwaka.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha ACT Wazalendo wilaya ya Kasulu Haruna Kwasakwasa, amesema uwepo wa mkurugenzi huyo umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato ya halmashauri hiyo ukilinganisha na kipindi cha nyuma.

Mwenyekiti wa Chama Cha ACT Wazalendo wilaya ya Kasulu, Haruna Kwasakwasa, Picha na Hagai Ruyagila

Hata hivyo, amesisitiza kuwa ni muhimu mapato yanayopatikana yakatumike kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuendelea kuboresha huduma za kijamii na maendeleo kwa wananchi wa Kasulu.