Joy FM
Joy FM
8 July 2026, 11:42

Ukatili wa kijinsia ni tatizo linaloathiri wanawake, wanaume na watoto katika jamii na kwa muda mrefu, jamii imekuwa ikielekeza zaidi macho kwa ukatili dhidi ya wanawake, hali iliyowafanya baadhi ya wanaume wanaopitia ukatili kushindwa kutoa taarifa kwa hofu ya kudharauliwa au kutokuaminiwa.
Na Filbert Gabriel
Wanaume Mkoani Kigoma wametakiwa kutoa taarifa za matukio ya ukatili yanayotokea katika jamii badala ya kukaa kimya, ili kuchangia kujenga kizazi bora cha baadaye na kuendeleza juhudi za kumlinda na kumlea mtoto wa kiume.
Akizungumza katika mahojiano maalumu yaliyofanyika kwenye studio za Radio Joy Fm, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Kigoma, Efeta Msiga, amesema baba ndiye nguzo ya familia, hivyo ana wajibu wa kujilinda, kuilinda familia yake na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili wa kijinsia vinapotokea.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Kigoma, Amina Kaniki, amesema wanaume hukumbwa na aina mbalimbali za ukatili ikiwemo ukatili wa kihisia na kimwili huku akihimiza kujitokeza hadharani na kutoa taarifa wanapofanyiwa au wanaposhuhudia vitendo vya ukatili.
Kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kigoma, ASP Michael Mjema, amesema wanaume wanapaswa kufika katika ofisi za Dawati la Jinsia na Watoto kutoa taarifa za vitendo vya ukatili wanapovikumbana navyo au kushuhudia wengine wakifanyiwa, badala ya kuwa na mtazamo kwamba huduma za dawati hilo zinawanufaisha wanawake pekee.
Mkoa wa Kigoma unaendelea kukabiliwa na changamoto ya matukio ya ukatili dhidi ya watoto wa kiume, hususan vitendo vya ulawiti ambavyo, katika baadhi ya matukio, hufanywa na watu wa karibu na waathirika na hali hiyo inaelezwa kuwa tishio kwa ustawi wa watoto hao na maendeleo ya familia pamoja na jamii kwa ujumla.