Joy FM
Joy FM
17 August 2026, 08:22

Usafi wa mazingira ni jambo muhimu sana katika maisha ya kila siku na kila mtu ana wajibu wa kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama na hii ni muhimu zaidi katika maeneo ya sokoni kwa sababu sokoni hukusanyika watu wengi na huuzwa vyakula na bidhaa mbalimbali ambazo zinazalisha uchafu
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mkoani Kigoma Dkt. Rashid Chuachua amewahimiza wananchi na wafanyabiashara wa soko la Nazareth lililopo Manisapaa ya Kigoma Ujiji kuchangamkia fursa ya kiuchumi inayotokana na taka kwa kuzitenganisha, kuzichakata na kuzipa thamani.
Dkt. Chuachua ametoa rai hiyo leo Agost 15 wakati aliposhiriki zoezi la usafi wa mazingira katika soko la Nazareth zoezi ambalo limeambatana na uzinduzi wa kampeni ya “TAKA NI PESA”, inayotekelezwa na Shirika la CRS kwa usaidizi wa kampuni ya JIDI inayotoa utaalamu wa kitaalamu.

Amesema kampeni hiyo, pamoja na kusaidia kuweka mazingira safi kwa kukusanya taka katika maeneo ya biashara, makazi na mikusanyiko ya watu, itawawezesha wananchi kujipatia kipato kupitia uchumi rejeshi kwa kuzitenganisha na kuzichakata taka.
“Wananchi tusione taka kama uchafu usio na thamani, bali tuzichukulie kama fursa ya kiuchumi tukizitenganisha, kuzichakata na kuzipa thamani, tunaweza kujiongezea kipato huku tukilinda mazingira,” amesema Dkt. Chuachua.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa shirika la CRS Joshua Charles amesema kuwa kampeni ya TAKA NI PESA inalenga kuwainua vijana na wanawake ili waweze kujikwamua kiuchumi kwa kuzigeuza taka kuwa fursa ya kujiongezea kipato kupitia mradi wa VOICES unaotekelezwa Tanzania na Zambia.
“taka zimekuwa ni changzo cha magonjwa na uchafuzi wa vyanzo vya maji na hivyo tumeona ni muhumu kuhakikisha tunatumia taka kuwa chanzo cha mapato kwa kuzitenganisha” amesema Charles.
Baadhi ya wananchi na wafanyabiashara katika eneo la Nazareth akiwemo Aron Misigalo wamesema kampeni hiyo ya TAKA NI PESA itasaidia kupunguza mrundikano wa takataka zilikuwa zinazagaa mtaani na kusababisha magonjwa kwa wananchi.
Mradi wa VOICES unatekelezwa Tanzania na Zambia kwa lengo la kuhamasisha mabadiliko ya tabia katika utunzaji wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.