Joy FM
Joy FM
22 July 2026, 07:53

Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya Uvinza Mkoani Kigoma limetakiwa kuendelea kushirikiana katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ili kusaidia katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo
Na Mwandishi weu
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza kwa kupata hati safi katika ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025 pamoja na kupunguza idadi ya hoja za ukaguzi, hatua inayoashiria kuimarika kwa usimamizi wa fedha za umma na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani, Balozi Sirro amewataka madiwani kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata zao, kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa, na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo.

Aidha, Balozi Sirro amesisitiza umuhimu wa kuendeleza zoezi la uandikishaji wa makazi, kuongeza juhudi za ukusanyaji wa mapato kupitia ulipaji wa kodi, kubuni vyanzo vipya vya mapato, kushirikiana kudhibiti wahamiaji haramu, pamoja na kuzuia migogoro ya ardhi ambayo inaweza kuhatarisha amani na kuchelewesha maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mh. Dinah Mathamani, amesema Halmashauri imeendelea kuchukua hatua za kurekebisha mapungufu yaliyobainishwa na ukaguzi wa CAG, na kwamba ufuatiliaji wa karibu utaendelea kufanyika ili kuhakikisha hoja zilizobaki zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati na kuimarisha zaidi utendaji wa Halmashauri.

Aidha amemshauri Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, kuendelea kulipa madeni ya wadau mbalimbali ili waweze kuendeleza utoaji huduma na kuondoa malalmiko yasiyokuwa ya lazina.
Kwa upande wao, baadhi ya Madiwani wamemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Uvinza kuchukua hatua ili kufuta hoja ya uwepo wa baadhi ya watumishi wenye sifa, wanaokaimu nafasi za ukuu wa Idara kwa muda mrefu bila kuthibitishwa kuwa wakuu wa Idara kamili.