Joy FM

Zaidi ya Tsh 122 milioni zajenga bwalo la chakula, jiko banifu Makere sekondari

9 September 2026, 15:48

Muonekano wa bwalo la shule ya sekondari Makere Wilaya ya Kasulu, Picha na Hagai Ruyagila

Uboreshaji wa miundombinu ya elimu inasaidia wanafunzi kupata mazingira rafiki ya kujinzia

Na Hagai Ruyagila

Mwenge wa uhuru 2026 umezindua na kukagua mradi wa ujenzi wa bwalo la chakula pamoja na majiko banifu katika Shule ya Sekondari Makere, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 122.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Makere, Abdon Bartazary, amesema ujenzi wa bwalo hilo umekamilika kwa asilimia 100 na tayari lipo tayari kutumika kwa shughuli zilizokusudiwa.

Mkuu wa shule ya sekondari Makere akisoma taarifa ya mradi, Picha na Hagai Ruyagila

Mbunge wa Jimbo la Kasulu Vijijini, Edibili Kazala, amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri hiyo, huku akiahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, amesema mradi huo umetokana na mapato ya ndani ya Halmashauri na kwamba Serikali itaendelea kupokea maelekezo ya Mwenge wa Uhuru kwa ajili ya kuboresha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mkuu wa Wilaya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu, Picha na Hagai Ruyagila

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, amesema Serikali imeendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya shule, hatua ambayo imekuwa chachu ya kuongeza mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.

Amesema bwalo hilo limejengwa kwa kuzingatia viwango vya ubora na litasaidia kuboresha mazingira ya wanafunzi katika Shule ya Sekondari Makere.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, Picha na Hagai Ruyagila