Joy FM

TAWLA yawajengea uwezo wanahabari kuripoti habari za ukatili Kigoma

25 June 2026, 12:58

Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali Mkoani Kigoma wakiwa kwenye mafunzo, Picha na Tryphone Odace

Ukatili wa kijinsia ni moja ya changamoto kubwa zinazoendelea kuathiri jamii nyingi nchini na vitendo hivi vinajumuisha ukatili wa kimwili, kingono, kisaikolojia na kiuchumi, ambavyo huathiri zaidi wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi

Na Tryphone Odace

Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari Mkoani Kigoma wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuripoti kwa weledi masuala ya ukatili wa kijinsia, mafunzo yaliyoandaliwa na Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA).

Baadhi ya wandishi wa habari Mkoani Kigoma wakiwa kwenye mafumbo, Picha na Tryphone Odace

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mwakilishi wa TAWLA Isabela  Nchimbi amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwapa waandishi wa habari uelewa mpana kuhusu namna ya kuandika na kuripoti habari za ukatili wa kijinsia kwa kuzingatia maadili ya taaluma, kulinda faragha za waathirika na kuepuka lugha zinazoweza kuongeza madhara kwa wahanga.

Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka TAWALA akizungumza wakati wa mafunzo, Picha na Tryphone Odace

Amesema vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia, kuhamasisha utoaji wa taarifa za vitendo vya ukatili pamoja na kuchangia mabadiliko ya mitazamo hasi inayochochea ukatili huo.

Naye Mkufunzi wa mafunzo hayo Prosper Kwigize amesema kuwa waandishi wa hbari hawana budi kujikita katika kuandika habari za ukatili wa kijinsia zenye manufaa kwa jamii kutokana na vitendo vya ukatili kuendelea kushamili kwenye jamii.

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kuboresha namna wanavyokusanya, kuandaa na kuripoti habari zinazohusu ukatili wa kijinsia kwa usahihi na weledi zaidi.

Waandishi wa habari kutoka Kigoma wakiwa katika mafunzo ya ukatili wa kijinsia Mjini Kigoma, Picha na Tryphone Odace

Wamesema mafunzo hayo pia yamewawezesha kuelewa sheria mbalimbali zinazolinda haki za wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi jambo litakalowasaidia kuandaa habari zenye kuhamasisha upatikanaji wa haki kwa waathirika.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza uwezo wa vyombo vya habari katika kuibua na kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia kwa njia inayochangia kinga, elimu na upatikanaji wa haki kwa waathirika.