Joy FM

TRA kuzindua mkakati wa kukuza wafanyabiashara wadogo Kigoma

24 June 2026, 14:34

Meneja wa TRA Mkoa Kigoma Beatus Nchota akiwa kwenye picha na baadhi wadau wengine, Picha na Mwandishi wetu

Wafanyabiashara wadogo ni nguzo muhimu katika maendeleo ya uchumi wa nchi yoyote na kundi hili linachangia kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji wa bidhaa, utoaji wa huduma na ajira kwa wananchi wengi

Na Mwandishi wetu

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kigoma inatarajia kuja na mpango mkakati maalumu unaolenga kuinua wafanyabiashara wadogo ili kukuza biashara zao na hatimaye kuingia kwenye mfumo rasmi wa ulipaji kodi.

Meneja wa TRA Mkoa wa Kigoma, Beatus Nchota, amesema hayo akikabidhi ssamani za ofisi kwa Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) Halmashauri ya wilaya Kigoma mkoani Kigoma na kueleza kuwa elimu ya biashara itakuwa nyenzo kuu ya kufanikisha mpango huo unaotarajia kuanza Julai Mosi mwaka huu.

Meneja wa TRA Mkoa Kigoma Beatus Nchota, Picha na Mwandishi wetu

Akizungumza na wafaanyabiashara hao Nchota alisema kuwa mamlaka hiyo imebaini kuwa wafanyabiashara wengi wadogo wana uwezo wa kukuza biashara zao lakini wanakabiliwa na changamoto za uelewa wa masuala ya usimamizi wa biashara, utunzaji wa kumbukumbu za mapato na matumizi pamoja na fursa za masoko.

“Lengo letu si kukusanya kodi pekee, bali pia kuona wafanyabiashara wanakua kiuchumi. Tunapotumia elimu ya biashara kuwajengea uwezo, tunawawezesha kuongeza mauzo, kupata faida zaidi na hatimaye kuingia kwenye wigo wa ulipaji kodi kwa hiari,” alisema Nchota.

Akizungumzia msaada wa samani uliotolewa kwa Shirikisho hilo la Umoja wa Machinga Meneja huyo wa TRA amesema kuwa unalenga kuwatia moyo na kuwaunga mkono ili biashara zao zikue na kuweza kulipa kodi Zaidi kwa biashara wanazofanya kwani hata sasa wanaponunua bidhaa hizo na kuja kuuza pia zimekuwa zikikatwa kodi.

Baadhi ya wanakikundi wakiwa katika picha ya pamoja na Meneja wa TRA Mkoa wa Kigoma, Picha na Mwandishi wetu

Wakizungumza baada ya kupokea samani hizo viongozi wa SHIUMA Halmashauri ya wilaya Kigoma akiwemo Mwenyekiti wa Umoja huo, Zuwena Hussein alisema kuwa kwa sasa TRA imekuwa ikifanya kazi kama mshirika kwa kusikiliza changamoto za biashara wanapokuja kwenye biashara zao badala ya kuwa taasisi ya usimamizi pekee si kama ilivyokuwa hapo awali jambo linalochangia wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari na kuwepo kwa ongezeko la walipa kodi wapya.