Joy FM

Milioni 600 kukamilisha kituo cha afya Kazuramimba Uvinza

25 May 2026, 08:01

Wananchi wa Kata ya Kazuramimba wakiwa kwenye mkutano wa hadhara na Mbunge Nuru Kashakari, Picha na Timotheo Leonard

Afya ni msingi muhimu katika maisha ya mwanadamu na jamii yenye watu wenye afya bora huwa na maendeleo mazuri kiuchumi, kijamii na kielimu

Na Timotheo Leonard

Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, Nuru Issa Kashakari, amewashukuru wananchi wa Kijiji cha Kazuramimba, Kata ya Kazuramimba, kwa kumuamini na kumchagua kuwa mbunge wao huku akiahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo upatikanaji wa kituo cha afya katika eneo hilo.

Mheshimiwa Kashakari ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kazuramimba, ambapo amesema zaidi ya shilingi milioni 600 zimeletwa kukamilisha kituo hicho ili kuondoa adha ya upatikanaji wa huduma za afya karibu.

Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, Nuru Issa Kashakari akiwa kwenye mkutano wa hadhara Kazuramimba, Picha na Timotheo Leonard

Hata hivyo katika kuhakikisha Jimbo la kigoma kusini linapata maendeleo , Mh. Kashakari amesema serikali tayari imeweka kwenye mipango ujenzi barabara ya Simbo kwenda Kalya pamoja na daraja la Mto Malagarasi, hatua ambayo inalenga kupunguza changamoto za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa eneo hilo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Salvatory Motto amemuuomba mbunge kuendelea na jitihada za kuwawakilisha wananchi ILI MIRADI mingi iendelee kutekelezwa.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Kazuramimba wameeleza faida za kukamilika kwa kituo cha afya cha Kazuramimba.

Wananchi wa Kata ya Kazuramimba wakiwa kwenye Mkutano wa hadhara ambao umeitishwa na Mbunge, Picha na Timotheo Leonard

Aidha, huu ni mkutano wa kwanza kwa mbunge huyo kukutana na wananchi wa Kata ya Kazuramimba tangu alipochaguliwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, ambapo wananchi walipata fursa ya kuzungumza naye na kuwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili.