Joy FM

Serikali yaimarisha ushirikiano na mashirika kukuza maendeleo Kakonko

13 August 2026, 16:35

Baadhi ya wajumbe walioshiriki kikao na wadau wa mashirika. Picha na Mwandishi wetu

Ushirikiano kati ya serikali na wadau wa maendeleo husaidia kuchochea utoaji wa huduma kwa wananchi

Na Mwandishi wetu

Serikali ya Wilaya ya Kakonko imeendelea kuimarisha ushirikiano na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa lengo la kuongeza ufanisi wa miradi ya maendeleo, kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha shughuli zinazotekelezwa na mashirika hayo zinatoa matokeo yanayoonekana kwa wananchi.

Hayo yameelezwa leo Agosti 13, 2026 wakati wa kongamano la mashirika yasiyo ya kiserikali lililofanyika katika Ukumbi Mpya wa Mikutano wilayani Kakonko, likiwa na lengo la kutathmini utekelezaji wa shughuli zao, kujadili mafanikio na kubaini changamoto zinazohitaji ufumbuzi ili kuongeza mchango wao katika maendeleo ya jamii.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Col. Evance Mallasa, amesema mashirika yasiyo ya kiserikali ni nguzo muhimu katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuleta maendeleo, kwa kuwa shughuli zinazotekelezwa na mashirika hayo zinagusa maisha ya wananchi na kuchangia katika kupunguza umaskini.

Col. Mallasa amesema kongamano hilo ni fursa ya kujifunza mbinu bora za utekelezaji, kubadilishana uzoefu na kuimarisha matumizi yenye tija ya rasilimali, akisisitiza kuwa fedha na rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinapaswa kusimamiwa kwa uadilifu na kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi.

“Hakikisheni rasilimali hususani fedha zinasimamiwa kwa uadilifu na kuleta matokeo yanayoonekana,” amesema Col. Mallasa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Isabella Mwakabonga, amesema ni muhimu mashirika kuwa na lugha moja na ufahamu wa pamoja katika utekelezaji wa shughuli zao, hatua ambayo itasaidia kuimarisha ushirikiano na kuongeza ufanisi wa kazi zinazofanyika kwa ajili ya wananchi.
Aidha, Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Kakonko, Ndg. Mustapha Mtungwe, ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali yanapopewa kibali cha kutekeleza shughuli zao wilayani humo kuhakikisha yanatoa taarifa kwa mamlaka na wadau wanaohusika na utekelezaji wa miradi, ili kuwezesha uratibu, ufuatiliaji na ushirikiano katika shughuli za maendeleo.

Kongamano hilo pia limetoa fursa kwa wawakilishi wa mashirika mbalimbali, yakiwemo Good Neighbour, REDESO, Mudewa, Nyakitoto Youth Development, Restless Development, Namwajafo, Tist, Rerai na Tamau, kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli zao katika jamii, mafanikio waliyopata, fursa zilizopo pamoja na changamoto na mapendekezo ya namna ya kuzitatua.

Kwa ujumla, kongamano hilo limeweka msisitizo katika kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali, huku likilenga kuhakikisha rasilimali na jitihada zinazowekezwa katika miradi ya maendeleo zinatafsirika kuwa matokeo halisi na yenye tija kwa wananchi wa Kakonko.