Joy FM

Wazazi wakabidhi madawati 100 kwa wanafunzi shule ya msingi Titye Kasulu

27 August 2026, 14:25

Baadhi ya madawati yaliyotengenezwa na wazazi kwa ajili ya wanafunzi shule ya msingi Titye, Picha na Emmannuel Kamangu

Kutengeneza madawati huwasaidia wanafunzi kupata sehemu nzuri ya kukalia wakati wa masomo badala ya kukaa sakafuni, wanafunzi hukaa kwenye madawati na hivyo kuwa tayari kujifunza

Na Emmanuel Kamangu

Wazazi na walezi wa shule ya msingi  titye kata ya titye  Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu wametengeneza  madawati 100 na kuyakabidhi kwa shule  hiyo ili kukabiliana na wimbi la watoto  kukaa chini wakati wa ujifunzaji.

Akizungumza mgeni rasmi wa hafla hiyo Bw. Respice Swetu  kwa niaba ya Afisa Elimu msingi Wilaya ya Kasulu amewataka wazazi na walezi kuendelea kuwa na mtazamo chanya ili kuendelea kushirikiana na  serikali katika  kutekeleza shuguli za maendeleo.

Naye  Afisa Elimu kata ya Titye Bw. Yoabu  Hinyula amewapongeza wazazi na walezi kwa umoja wao huku akibainisha kuwa madawati hayo yatapunguza utoro kwa kiasi kikubwa.

Aidha mkuu wa shule ya msingi Titye Bw. Hilali  Abudala amesema shule hiyo  inakabiliwa na uhaba wa madawati 349 na kuwa kukamilika kwa madawati 100 kutafanya shule hiyo kubaki na uhaba wa madawati 249 na kuwaomba wananchi na wadau wengine wa maendeleo kuendelea kushirikiana ili kumaliza kabisa kero hiyo.

Wanafunzi pamoja na mgeni rasmi Bw, Respice Swetu akiwa na wanafunzi wa shule ya msingi Titye katika madawati mapya baada ya kukabidhiwa, Picha na Emmanuel Kamangu

Kwa upande wao wazazi na walezi wa shule ya msingi titye wamesema wamewiwa kuchangishana fedha kwaa ajili ya kutengeneza madawati baada ya kuona watoto wao wakipitia adha kubwa ya kukaa chini wakati wa ujifunzaji na kushindwa kujifunza kwa ufanisi.

Madawati hayo 100 yamegharimu jumla ya kiasi cha Tsh million 3 na laki 1 ikiwa ni michango ambayo imetokana na jasho la wananchi ili kuhakikisha watoto wao wanasoma wakiwa katika mazingra rafiki.

Sauti ya Emmanuel Kamangu Mwandishi wa habari Joy Fm Kasulu