Joy FM
Joy FM
16 April 2026, 11:38 am

Mnamo Disemba 2023, aliteuliwa kuwa Kamishna katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (CENI), ambapo alisimamia masuala ya ugavi na maandalizi ya uchaguzi.
Na Bukuru Daniel
Waziri wa Habari na Mawasiliano, Gabby Bugaga, amekutwa ndani ya gari akiwa amefariki dunia Aprili 16, katika shamba la michikichi lililopo Kivoga, eneo la Rubirizi katika wilaya ya Ntahangwa, mkoani Bujumbura.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa eneo hilo, mwili wake ulipatikana akiwa peke yake ndani ya gari, bila dereva wala mlinzi wa karibu. Pia inaripotiwa kuwa gari hilo lilikuwa na dalili za kuharibika, hali ambayo imezua maswali mengi kuhusu mazingira ya tukio hilo.
Serikali ya Burundi ilimteua Gabby Bugaga mwaka 2025 kuwa waziri wa mawasiliano na Vyombo vya Habari, katika mabadiliko mapya ya uongozi wa sekta ya habari na mawasiliano nchini humo.
Bugaga, ambaye anatoka katika eneo la Muhuta, mkoa wa Bujumbura, alikuwa mtaalamu mwenye uzoefu mpana katika masuala ya mawasiliano ya umma na uandishi wa habari. Alisomea sayansi ya mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Lumière cha Bujumbura kabla ya kuanza kazi yake katika vyombo vya habari vya umma.
Katika hatua za awali za kazi yake, alifanya kazi katika vyombo vya habari vya taifa, ambako alijijengea sifa kama mwandishi na mtaalamu wa mawasiliano. Mwaka 2013, alitunukiwa tuzo na baraza la Kitaifa la Mawasiliano (CNC) kutokana na makala yake iliyohusu juhudi za upandaji miti katika eneo la Butihinda, baada ya uharibifu wa mazingira uliosababishwa na uchimbaji holela wa dhahabu.
Baadaye, alihamia katika nafasi za mawasiliano ndani ya taasisi za serikali, akihudumu kama msemaji wa Bunge la Seneti, kisha mkuu wa mawasiliano katika Seneti, na baadaye kuwa msemaji wa Spika wa Seneti ya Burundi.
Uteuzi wake kuwa Waziri wa Mawasiliano na Vyombo vya Habari ulitajwa na wachambuzi kuleta uzoefu mkubwa na mabadiliko katika mawasiliano ya kitaasisi serikalini.