Joy FM

Wanawake wanahabari wajengewa uwezo kukabiliana na vitisho vya kidijitali Morogoro

10 July 2026, 07:55

Baadhi ya waandishi wa habari wanawake wakiwa kwenye picha ya pamoja, Picha na Mwandishi wetu

Katika dunia ya sasa, maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano yamebadilisha kwa kiasi kikubwa namna wanahabari wanavyokusanya, kuchakata na kusambaza habari na majukwaa ya kidijitali yamekuwa nyenzo muhimu katika kazi ya uandishi wa habari, pamoja na fursa hizo, yameibuka pia vitisho vya kidijitali vinavyowaathiri wanahabari, hususan wanawake

Na Mwandishi wetu

Wakati matumizi ya teknolojia yakizidi kuwa sehemu muhimu ya kazi za uandishi wa habari, waandishi wa habari wanawake 22 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wamepatiwa mafunzo ya usalama wa kidijitali ili kuwawezesha kulinda taarifa zao, vyanzo vya habari na usalama wao wanapokuwa mtandaoni.

Mafunzo hayo ya siku nne yaliyoandaliwa na Union of Tanzania Press Clubs (UTPC) yamefanyika mkoani Morogoro kuanzia Julai 6 hadi Julai 9, 2026, yakilenga kuwajengea uwezo washiriki kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto zinazotokana na matumizi ya majukwaa ya kidijitali.

Mkurugenzi wa UTPC, Kenneth Simbaya, Picha na Mwandishi wetu

Kupitia mafunzo hayo, waandishi hao wamejifunza masuala mbalimbali ikiwemo ulinzi wa vifaa vya kidijitali, matumizi ya nywila imara na Two-Factor Authentication (2FA), usalama wa mitandao ya kijamii, mawasiliano salama, digital hygiene, ulinzi wa vyanzo vya habari na mafaili, pamoja na namna ya kukabiliana na mashambulizi ya mtandaoni.

Washiriki pia wamepata uelewa kuhusu matumizi ya zana za kuongeza usalama wa kidijitali ikiwemo VPN kwa matumizi salama ya Wi-Fi za umma, pamoja na njia za kulinda faragha na utambulisho wao katika mazingira ya mtandaoni.

Baadhi ya waandishi wa habari wanawake wakiwa kwenye picha ya pamoja, Picha na Mwandishi wetu

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mkurugenzi wa UTPC, Kenneth Simbaya, amewataka washiriki kuhakikisha maarifa waliyoyapata yanakuwa sehemu ya mabadiliko katika kazi zao za kila siku na si kubaki kuwa nadharia.

Amesisitiza kuwa waandishi wanapaswa kutumia ujuzi huo kama nyenzo muhimu katika kuimarisha uandishi wa habari wa kidijitali, huku wakiendelea kuwaelimisha waandishi wenzao na hadhira zao kuhusu umuhimu wa usalama wa kidijitali.

“Maarifa haya yanapaswa kwenda zaidi ya washiriki waliopo hapa. Kila mmoja ana nafasi ya kuwa mhamasishaji wa mabadiliko kwa kuwafikia wengine kupitia kazi zake za kihabari na majukwaa ya kidijitali,” amesema.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo Iman Luvanga, Picha na Mwandishi wetu

Mafunzo hayo yanatajwa kuwa hatua muhimu katika kuwawezesha waandishi wa habari wanawake kufanya kazi katika mazingira salama zaidi ya kidijitali, hasa katika kipindi ambacho mashambulizi ya mtandaoni yanaendelea kuongezeka.