Joy FM

Kandahari kupigania barabara ya lami Simbo–Kalya Uvinza

13 May 2026, 15:19

Mbunge wa jimbo la Kigoma Kusini Mhe. Nuru Issa Kashakari, maarufu Kandahari, Picha na Mtandao

Mbunge wa jimbo la Kigoma Kusini Mhe. Nuru Issa Kashakari maarufu Kandahari amewataka wananchi wa jimbo hilo kutokata tamaa huku akiahidi  kupambana hadi kupatikana kwa barabara ya lami kutoka Simbo kwenda Kalya kwani ujenzi wa miundombinu hiyo ni moja ya vipaumbele vyake vikuu ili kuchochea usafiri na uchumi kw wananchi.

Mheshimiwa Kashakari ameyasema hayo leo wakati akizungumza kwa njia ya simu na Redio Joy FM, kupitia kipindi cha Good Morning Kigoma.

Katika mahojiano hayo, Mbunge Nuru Kashakari amesisitiza kuwa kiu yake kubwa ni kuona barabara hiyo ya kimkakati inajengwa kwa kiwango cha lami ili kuondoa kero ya usafirishaji na usafiri inayowakabili wananchi kwa muda mrefu.

Sauti ya Mbunge wa jimbo la Kigoma Kusini Mhe. Nuru Issa Kashakari, maarufu Kandahari

Mbali na barabara hiyo, Mhe. Kashakari ameiomba serikali kuelekeza nguvu  kwenye ujenzi wa daraja la Mto Malagarasi linalounganisha maeneo ya Ilagala na Kajeje, ili kubadilisha maisha wananchi wa maeneo hayo ambao wamekuwa wakiteseka kuvuka mto huo.

Sauti ya Mbunge wa jimbo la Kigoma Kusini Mhe. Nuru Issa Kashakari, maarufu Kandahari

Katika hatua nyingine, Mbunge Kandahari ameweka wazi jitihada zake binafsi katika kuboresha sekta ya elimu jimboni humo ambapo amesema hadi hivi sasa amechangia takribani madawati 600 ili kuondoa changamoto ya watoto kukosa madawati.