Joy FM
Joy FM
1 July 2026, 12:48

Taifa lenye amani na utulivu hujengwa kwa ushirikiano wa wananchi, viongozi na taasisi mbalimbali za kijamii, ikiwemo taasisi za dini na mojawapo ya njia zinazotajwa kuchangia ustawi wa taifa ni kuwaombea viongozi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, hekima na uwajibikaji.
Na Sadick Kibwana
Wakazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mkoani Kigoma, wamehimizwa kuendelea kuwaombea viongozi wa kitaifa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, hekima na kwa kuzingatia mamlaka waliyopewa.
Wito huo umetolewa katika Kongamano la Maombi kwa Viongozi wa Nchi na Wananchi, lililoandaliwa na Kanisa la Kipentekoste Nuru ya Ulimwengu – Mji wa Makimbilio.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mtume Christopher Aldoph Kibambi amesema kuwa wananchi wana wajibu wa kuliombea taifa pamoja na viongozi wake ili waendelee kuliongoza taifa kwa uadilifu, haki na hofu ya Mungu.

Naye Mwakilishi wa Serikali, Bw. Gama A. Gama, amelipongeza Kanisa la Mji wa Makimbilio kwa kuandaa kongamano hilo, akisema limekuwa na manufaa kwa wakazi wa Kigoma na limeendelea kuhimiza mshikamano na maadili katika jamii.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria kongamano hilo wamesema maombi ya pamoja kwa ajili ya taifa na viongozi wake ni muhimu katika kuimarisha amani, umoja na maendeleo ya nchi.
Kongamano hilo ni sehemu ya mwendelezo wa maombi yanayolenga kuliombea Taifa, viongozi wake pamoja na kudumisha amani na utulivu, ili shughuli za maendeleo ziendelee kufanyika katika mazingira ya utulivu na mshikamano.