Joy FM

Viongozi wa dini wapewa elimu ya kujikinga na ebola Kigoma

22 July 2026, 14:20

Baadhi ya wajumbe wakiwa katika semina ya uelewa kuhusu namna ya kukabiliana na ebola, Picha na Mwandishi wetu

Elimu ya kujikinga ya ugonjwa wa ebola imeendelea kutokelewa kwa jamii ili kuhakikisha wananchi wanachukua tahadhali za kujikinga na ugonjwa wa ebola na mpaka hakuna taarifa za uwepo wa ugonjwa huo nchini

Na Mwandishi wetu

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dkt. Damas Kayera amesema mkoa huo umechukua tahadhari mbalimbali za kujiandaa kukabiliana na milipuko ya magonjwa ya kuambukiza, ikiwemo Ebola na magonjwa mengine yanayofanana

Dkt. Kayera amesema hayo katika mahojiano maalum na wataalamu wa Wizara ya Afya wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa dini, wazee wa mila, waandishi wa habari na watu mashuhuri katika jamii, wakati wa mafunzo maalum yaliyoandaliwa baina ya Serikali na CIHEB Tanzania amesema kutokana na jiografia ya Kigoma kuwa ni miongoni mwa mikoa inayopakana na nchi jirani, Serikali ya mkoa ilianza kuchukua hatua za tahadhari mara baada ya kupokea taarifa za tishio la mlipuko wa Ebola katika nchi jirani.

“Mkoa wa Kigoma ukiwa ni miongoni mwa mikoa ya mipakani, tayari tumechukua tahadhari muhimu tangu tulipopata taarifa za tishio la Ebola katika nchi jirani. Watumishi wote wa afya kuanzia ngazi ya msingi, vituo vya afya hadi Hospitali wamepewa mafunzo na elimu ya utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo,” amesema Dkt. Kayera

Baadhi ya viongozi wa dini na wadau wengine wakiwa katika kikao cha uelewa wa kukabiliana na ebola, Picha na Mwandishi wetu

Aidha, amesema mkoa umeimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwemo Idara ya Uhamiaji, ambazo zinafanya kazi katika maeneo yote ya mipaka ya kuingia na kutoka nchini ili kuimarisha ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza.

Dkt. Kayera amesema wataalamu wa afya waliopo katika maeneo ya mipakani wamewezeshwa vifaa maalumu vya uchunguzi kwa wasafiri wanaoingia nchini, ambapo mtu yeyote atakayebainika kuwa na dalili za ugonjwa huo huwekwa chini ya uangalizi maalumu kwa mujibu wa miongozo ya afya.

Kwa upande wake, Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma Mkoa wa Kigoma, Abedi Michael, amesema hadi sasa zaidi ya wataalamu 300 wa afya kutoka vituo mbalimbali vya kutolea huduma wamepatiwa mafunzo ya kujikinga na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Ameongeza kuwa, mbali na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya, mkoa umefanikiwa pia kutoa mafunzo kwa zaidi ya wahudumu 280 wa afya ngazi ya jamii pamoja na kusambaza mabango na vipeperushi vyenye ujumbe wa kuelimisha wananchi.

Baadhi ya viongozi wa dini wakiwa kwenye kikao cha elimu ya uelewa wa kukabiliana na ebola, Picha na Mwandishi wetu