Joy FM
Joy FM
9 October 2026, 00:20

Katika makabidhiano hayo suala la usimamizi wa miradi ya maendeleo limetiliwa mkazo ili kuhakikisha Halmashauri ya Kasulu inaendelea kufikisha huduma kwa wananchi
Na Mwandishi wetu
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera, Kanali Isaac Mwakisu, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Luteni Kanali Joseph Murimi, kusimamia kwa karibu miradi yote ya kimkakati inayotekelezwa wilayani humo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati.
Akitoa taarifa ya Wilaya ya Kasulu katika kikao cha makabidhiano ya ofisi, Kanali Mwakisu amesema miradi hiyo inahitaji usimamizi wenye weledi ili kuhakikisha inakamilika na kuleta tija kwa wananchi.

Kanali Mwakisu amesema Wilaya ya Kasulu ina miradi mingi ya maendeleo na kimkakati ambayo bado haijakamilika,hivyo ni muhimu kufuatilia hatua za utekelezaji wake ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Luteni Kanali Joseph Murimi, ameahidi kushirikiana na watumishi wa wilaya hiyo katika kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora ili kuharakisha maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.

Aidha Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya Kasulu Mbelwa Chidebwe amesema wataendelea kutoa ushirikiano kwa mkuu huyo wa wilaya ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu ya kuwahudumia wananchi kwa wakati ikiwa ni pamoja na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo iweze kukamilika kwa wakati.