Joy FM

Fainali ya Mayeye CUP yaingia dosari

19 October 2026, 09:13

Muonekano wa kombe alilotakiwa kukabidhiwa mshindi wa fainali ya Mayeye CUP, Picha na Sadick Kibwana

Mchezo wa fainali kati ya Mwandiga United dhidi ya Majengo sokoni umeshindwa kufanyika baada ya kubainika kukiukwa kwa baadhi ya kanuni za uendeshaji wa mashindano hayo

Na Sadick Kibwana

Fainali ya ligi ya Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, Kiza Hussein Mayeye – Mayeye CUP 2026, imeshindwa kutamatika baada ya kutokea sintofahamu ya kikanuni katika mchezo huo uliotakiwa kufanyika katika uwanja wa tarafa ya Mwandiga ukizikutanisha Mwandiga United dhidi ya Majengo Sokoni ulisitishwa dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza.

Akizungumza na waandishi, Katibu wa chama cha soka Wilaya ya Kigoma, Dumango Yahya, amesema mgogoro umemhusisha mchezaji wa Mwandiga United anayedaiwa kuchezea timu nyingine tofauti katika mashindano hayo kabla ya fainali, jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za mashindano.

Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Mwandiga United, Mussa Jumanne Ramadhani, amekanusha madai hayo akisema mchezaji huyo hakucheza mchezo wowote na timu nyingine, bali wapinzani wao walimfuata na yeye akawakataa, ndipo chanzo cha vurugu hizo.

Kocha Msaidizi wa Mwandiga United, Mussa Jumanne Ramadhani, Picha na Sadick Kibwana

Naye Kocha wa Majengo Sokoni, Maulid Ally, amesema wao walimfuata awali kocha wa mchezaji huyo kutoka Timu ya Kasaka na akakiri kumchezesha mchezaji huyo katika mashindano hayo.

Kocha wa Majengo sokoni Maulid Ally, Picha na Sadick Kibwana

Kamati ya mashindano imesema itakaa kwa dharura kupitia kanuni na taarifa muhimu ili kujiridhisha na kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu hatima ya fainali hiyo.