Joy FM

ALAT Mkoa yaridhishwa na utekelezaji wa miradi Uvinza

5 November 2026, 10:13

Baadhi ya wajumbe wa ALAT Mkoa wa Kigoma wakiwa wakiwa katika ziara ya kukagua miradi, Picha na Mwandishi wetu

Halmashauri ya Wilaya Uvinza Mkoani Kigoma imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imesaidia kusogeza huduma kwa wananchi

Na Mwandishi wetu

Ujumbe wa ALAT Mkoa wa Kigoma umetembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, huku ukieleza kuridhishwa na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Kigoma, Mh. Alex Baragomwa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, amepongeza juhudi zinazofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza katika kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Wajumbe wa ALAT Mkoa wakiwa wametembelea miradi Uvinza, Picha na Mwandishi wetu

Mh. Baragomwa mesema ziara hiyo imewapa fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu namna bora ya kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kuzingatia taratibu, viwango na thamani ya fedha.

Katika ziara hiyo, ujumbe umetembelea miradi ya sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Afya Kandaga wenye thamani ya Shilingi milioni 250, pamoja na upanuzi wa Kituo cha Afya Kazuramimba wenye thamani ya Shilingi milioni 619.6. Miradi hiyo inalenga kuboresha upatikanaji na utoaji wa huduma za afya kwa wananchi, hususan huduma za afya ya mama na mtoto.

Muonekano wa mradi mojawapo uliotembeleqa na ujumbe wa ALAT Mkoa, Picha na Mwandishi wetu

Aidha, ujumbe umetembelea mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya kwanza katika eneo la Lugufu wenye thamani ya Shilingi milioni 603.9, unaolenga kuboresha miundombinu ya elimu na kuweka mazingira bora kwa maandalizi ya udahili wa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza.

Pia umetembelea mradi wa ujenzi wa miundombinu ya shule katika Shule ya Msingi Shekeshe wenye thamani ya Shilingi milioni 342.9.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mh.Mtela Mwampamba, akifungua kikao cha kuukaribisha ujumbe wa ALAT mkoa katika Wilaya ya Uvinza amesema kuwa vikao na ziara hizo ni muhimu katika kujadili, kufanya maamuzi na kusimamia utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Halmashauri.

Kwa ujumla, miradi hiyo minne ina thamani ya Shilingi bilioni 1.816, ikiwa ni uwekezaji unaolenga kuboresha huduma za kijamii katika sekta za afya na elimu na kuongeza ustawi wa wananchi wa Wilaya ya Uvinza. Ziara hiyo pia imekuwa fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri hiyo.