Joy FM
Joy FM
6 November 2026, 15:16

Wakulima katika Halmashauri ya Wilaya Kasulu wamesema kuwa elimu ya kilimo bora ni muhimu na upatikanaji wa pembejeo kwa wakati itasaidia kuongeza uzalishaji wenye tija
Na Hagai Ruyagila
Maafisa Kilimo na ugani katika Halmashauri ya Mji Kasulu, mkoani Kigoma, wametakiwa kuendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu uzingatiaji wa kanuni bora za kilimo ili kuongeza tija katika uzalishaji na kuimarisha upatikanaji wa chakula.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Luteni Kanali Joseph Murimi, wakati akizungumza katika kikao cha Kamati ya Pembejeo cha Halmashauri ya Mji Kasulu, kilicholenga kubaini changamoto zinazokabili upatikanaji wa pembejeo za kilimo.

Amesema maafisa ugani wana jukumu muhimu la kuwaelimisha na kuwaongoza wakulima kutumia mbinu za kisasa za kilimo pamoja na kuzingatia kanuni bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kupata mavuno yenye tija.
Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Mifugo, Kilimo na Uvuvi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Sabinusi Chaula, ameeleza hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa wakati, akibainisha kuwa hadi sasa halmashauri hiyo imepokea mbolea kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulima.

Baadhi ya wakulima katika Halmashauri ya Mji Kasulu wameiomba Serikali kupitia idara ya kilimo kusimamia upatikanaji na uuzaji wa pembejeo kwa kuhakikisha wafanyabiashara wanazingatia bei elekezi iliyowekwa na Serikali ili kuwawezesha wakulima kupata pembejeo kwa gharama zinazostahili.