Joy FM
Joy FM
17 November 2026, 14:17

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma amewataka viongozi na watendaji katika ngazi zote kushirikiana na wawekezaji kuhakikisha wakulima wanapata elimu ya kutosha ili waweze kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa hewa ukaa.
Na Orida Sayon
Ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu hewa ukaa kwa wakulima Mkoani Kigoma umetajwa kuwa miongoni mwa changamoto zinazoweza kukwamisha utekelezaji wa miradi ya kilimo cha kaboni, licha ya kuwa na fursa kubwa za kuongeza kipato na kuboresha maisha ya wakulima.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao cha utambulisho wa mradi wa hewa ukaa katika halmashauri za Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Mkoa huo, Balozi Simon Sirro, amesema elimu kwa wakulima ni jambo muhimu katika kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.
Mradi huo unatekelezwa kupitia mfumo wa kilimo mseto unaohusisha mashamba ya mazao ya chakula, biashara na miti, chini ya usimamizi wa Kampuni ya KADERES.
Sirro amewataka viongozi na watendaji katika ngazi zote kushirikiana na wawekezaji wa mradi huo kuhakikisha wakulima wanafikiwa na kupatiwa elimu ya kutosha kuhusu fursa na manufaa ya kilimo cha kaboni.

Amesisitiza kuwa elimu hiyo itasaidia kufikia lengo la kusajili wakulima watakaoshiriki katika uzalishaji wa mazao ya biashara ya hewa ukaa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya KADERES kutoka Mkoa wa Kagera, Renald Faustine, amesema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali za kimataifa na ndani ya nchi.
Amezitaja taasisi hizo kuwa ni Rabobank, Acorn na Achmea Foundation za nchini Uholanzi, pamoja na Benki ya CRDB ya Tanzania.
Faustine amesema mradi huo umejikita katika kuwawezesha wakulima wadogo kushiriki katika soko la kimataifa la hewa ukaa, ambapo zaidi ya wakulima 100,000 wanatarajiwa kusajiliwa.
“Mradi huu umelenga kuwafikia wakulima wadogo na kuwaunganisha na fursa za soko la kimataifa la hewa ukaa, ambapo tunatarajia kusajili zaidi ya wakulima laki moja,” amesema Faustine.
Ameongeza kuwa mradi huo una malengo mapana yanayolenga kuboresha maisha ya wakulima na jamii kwa ujumla, ikiwemo kuongeza uhakika wa chakula, kuboresha lishe, kuongeza kipato cha kaya na kuwaunganisha wakulima wadogo na masoko ya kimataifa ya hewa ukaa (kaboni).
Kupitia kilimo mseto, wakulima wanapata fursa ya kuendelea kuzalisha mazao ya chakula na biashara huku wakishiriki katika shughuli zinazochangia kupunguza hewa ukaa na kuhifadhi mazingira.
Mradi huo unatajwa kuwa na nafasi ya kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wakulima wa Mkoa wa Kigoma endapo elimu, ushirikishwaji na utekelezaji wake vitazingatiwa kwa ufanisi.