Joy FM
Joy FM
20 August 2026, 07:50

Serikali imekuwa ikitoa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri kwa makundi mbalimbali, huku ikiweka msisitizo katika usimamizi na utoaji wa elimu kwa wanufaika ili kuhakikisha mikopo hiyo inaleta matokeo yaliyokusudiwa.
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Bi. Zainab Katimba, amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuendelea kutoa elimu na hamasa kwa wananchi, hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri.
Bi. Zainab ametoa wito huo Agosti 18, 2026, wakati wa ziara yake ya kutembelea vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vinavyonufaika na mikopo hiyo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Amesema Maafisa Maendeleo ya Jamii, kuanzia ngazi ya kata, wana wajibu wa kuwaelimisha wananchi kuhusu fursa hiyo pamoja na matumizi sahihi ya mikopo ili iweze kuchochea shughuli za kiuchumi na kuongeza kipato.
“Serikali itaendelea kutoa mikopo hiyo na kusimamia utekelezaji wake ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata fursa ya kutumia mitaji hiyo katika shughuli za uzalishaji” amesema Katimba.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri ametembelea vikundi vitano ambavyo ni Upendo Women, kinachojihusisha na ufumaji na uuzaji wa mashuka; Unique Women, kinachofanya ufugaji wa kuku wa nyama na mayai; Azania Bakery, kinachojihusisha na uuzaji wa vitafunwa; Lukundo, kinachotengeneza kinywaji cha tangawizi; na Tito Phone Accessories, kinachojihusisha na uuzaji na utengenezaji wa vifaa vya simu.

Wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapatia fursa hiyo, wakieleza kuwa imewawezesha kujiajiri, kuajiri wengine, kugharamia elimu ya watoto wao na kuboresha maisha yao kiuchumi.

Mikopo ya asilimia 10 hutolewa na Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuanzisha na kuendeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi.